NEWS

Monday, 2 March 2026

Tarime Vijijini: RC Mara asifu viwango miradi ya CSR Barrick, apokea nyumba pacha ya walimu Nyamongo Sekondari



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (suti ya rangi ya bluu), Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (suti ya rangi ya ugoro) na viongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, miongoni mwa wengine wakifurahia picha ya pamoja wiki iliyopita, wakati wa kukabidhi nyumba pacha ya walimu iliyojengwa kutokana na fedha za CSR Barrick katika Shule ya Sekondari Nyamongo.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
----------------

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameeleza kuridhishwa na viwango vya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Mgodi huo unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

“Kwa namna ya pekee nawapongeza Barrick kwa weledi uliotukuka,” RC Mtambi alisema Ijumaa iliyopita wakati akipokea nyumba pacha ya kisasa ya walimu ambayo imejengwa na mgodi huo katika Shule ya Sekondari Nyamongo kwa gharama ya shilingi milioni 124 kupitia CSR.

RC Mtambi alisema mradi huo umezingatia viwango vya kimataifa huku akiwapongeza wafanyakazi wa Barrick kwa kuendelea kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi ya CSR.

“Nimekagua na kuridhika kwamba mradi huu wa nyumba ya walimu upo kwenye viwango vizuri. Hongereni sana,” RC Mtambi alisema.

Mkuu huyo wa mkoa alisema miradi inayotekelezwa na kampuni ya Barrick katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ni kielelezo cha matunda ya sera nzuri za uwekezaji iliyoweka na Seriklali ya Tanzania.

“Hii ndiyo miradi ya kuleta Mwenge wa Uhuru imulike matunda ya sera nzuri ya uwekezaji,” alisema.

Aidha, RC Mtambi alieleza kufurahishwa na uamuzi wa kampuni ya Barrick kutumia wakandarasi wazawa katika kutekeleza miradi hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, alipongeza pia kampuni ya Barrick kwa kuendelea kutekeleza idadi kubwa ya miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

“Ninawashukuru sana watu wa Barrick, mtu akifanya jambo zuri apongezwe, wanafanya mambo kwa uwazi,” Waitara alisema kwa ufupi katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko.

Kwa mujibu wa taraifa ya GM Lyambiko iliyosoma na Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi, mbele ya Mkuu wa Mkoa, ujenzi wa nyumba hiyo ni miongoni mwa miradi mipya 51 ya CSR ambayo imekamilka kwa silimia 100, huku utekelezaji wa miradi mingine 52 ukiwa unaendelea katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

RC Mtambi aliimimia sifa kampuni ya Barrick kwa kuendelea kusimamia vizuri utekelezaji wa wa miradi hiyo ambayo inagharimu mabilioni ya fedha kutokana na uzalishaji wa dhahabu katika mgodi huo.

Barrick ilitumia zaidi shilingi bilioni 26.86 kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ipatayo 255 tangu mwaka 2019 ilipokabidhiwa kuendesha mgodi huo hadi sasa.

Sekta ya elimu inapewa sehemu kubwa ya bajeti ya CSR na mgodi huo ikifuatiwa na afya.

Lakini pia mgodi huo umendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya miundombinu ya barabara na maji katika vijiji vinavyouzunguka.

Mgodi huo unatenga dola sita kwa kila wakia (ounce) ya dhahabu unayozalisha kwa ajili ya miradi ya CSR.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages