NEWS

Friday 19 August 2022

Madiwani Tarime waibana TARURA kwa ubovu wa barabara




Na Mara Online News
-----------------------------

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, wamelalamikia ubovu wa barabara katika kata zao na kuitaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kueleza kinachoisababisha kutotatua tatizo hilo.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Simion Kiles Samwel ‘amepigilia msumari’ kwa kukiri kwamba barabara nyingi zimeharibika kiasi cha kutopitika kwa usafiri wa vyombo vya moto.

“Hali ya barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ni mbaya,” amesisitiza Kiles katika kikao cha baraza lao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari ya JK Nyerere, leo Agosti 19, 2022.

Baada ya malalamiko mengi kutoka kwa madiwani, Mwenyekiti Kiles amemuomba Meneja wa TARURA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Charles Marwa kutembelea kila kata ili kujionea hali ya ubovu wa barabara kwa hatua za ufumbuzi.

“Na katika hili ni vizuri Meneja atoe ratiba ya kutembelea kata zetu ili kila diwani ajue ni lini atakwenda katani kwake,” aliongeza Kiles.

Akijibu malalamiko hayo, Mhandisi Marwa amesema moja ya mambo yaliyompa wakati mgumu alipohamishiwa Tarime mwaka jana, ni kitendo cha mkandarasi kupewa kazi nyingi za matengenezo ya barabra, hali iliyosababisha miradi mingi ya mabilioni ya fedha kukwama.

“Kuna mkandarasi ameshikilia kata 10, amekwamisha miradi [matengenezo ya barabara] kwa muda mrefu. Nilipohamishiwa Tarime Januari 2021, nilikuta miradi yenye thamani ya shilingi zaidi ya bilioni tano imelala, lakini nimeikwamua,” amesema.


Mhandisi Marwa (kushoto) kikaoni

Hata hivyo, Meneja huyo wa TARURA amesema ametembelea kata tatu kati ya 26 zinazounda Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na kubaini kuwa barabara nyingi zinazolalamikiwai hazijaingizwa kwenye mpango wa kutengenezwa na Serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages