NEWS

Monday 29 August 2022

Mapya yabainika kiwanda cha nguzo za umeme Mara

Hii ndiyo hali halisi ya muonekano wa kiwanda hicho kwa sasa

Na Mwandishi Wetu, Mara
-----------------------------------

MWEKEZAJI wa kiwanda cha nguzo za umeme kinachojulikana kwa jina la Tarime Woods and Poles Treatment Plant Limited (TAWOODS), aliomba umeme kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho na siyo uzalishaji, Sauti ya Mara imebaini.

Uchunguzi uliofanywa na Sauti ya Mara wiki iliyopita, umebaini kuwa baada ya Shirika la Taifa la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kupata ombi hilo, lilimpelekea umeme kwa bajeti yake ili kuharakisha ujenzi wa kiwanda hicho katika kijiji cha Remagwe wilayani Tarime.

Aidha, katika kuhakikisha kiwanda hicho kinakuwepo ili kuchangia uchumi wa wananchi na mapato ya Serikali, siku chache zilizopita TANESCO ilipeleka transfoma nyingine kiwandani hapo, baada ya iliyokuwepo kuungua kwa kupigwa radi.

TANESCO imechukua hatua hiyo ili kunusuru kiwanda hicho, kwani tayari Mkurugenzi wake alikuwa na wazo la kukifunga kwa hofu kwamba angecheleweshewa transfoma ya umeme.

Mwekezaji wa kiwanda hicho, Peter Mwera, aliulizwa na Sauti ya Mara kwa njia ya simu wiki iliyopita na kukiri kupelekewa transfoma nyingine katika eneo la kiwanda hicho.

Alipoulizwa iwapo sasa atasitisha mpango wa kufunga kiwanda hicho baada ya kupelekewa transfoma hiyo, Mwera alijibu “Tutafanya kikao cha Bodi ya Wakurugenzi mwisho wa mwezi huu [Agosti 2022] na kutoa azimio.”

Hata hivyo, inaelezwa kwamba TANESCO iko tayari kumuunganishia umeme wenye uwezo wa kuendesha mitambo ya kiwanda hicho kwa ajili ya uzalishaji, mara baada ya ujenzi wa miundombinu yake kukamilika.

Sauti ya Mara ilitembelea kiwanda hicho hivi karibuni na kushuhudia nguzo kadhaa zilizovunwa kwenye mashamba ya mwekezaji huyo, ambazo hata hivyo zimeharibika kutokana na kuandaliwa kabla ya ujenzi wa mitambo ya kuzitibu kukamilika.

TANESCO) inaendelea kufanya jitihada za makusudi kuhamasisha na kuvutia wawekezaji wa viwanda mkoani Mara kwa maslahi mapana ya Taifa.

Uchunguzi zaidi umebaini kuwa wawekezaji wa viwanda ni miongoni mwa wateja wanaopewa kipaumbele katika kuunganishiwa huduma ya umeme mkoani hapa.

Inaelezwa kwamba uwazi wa wawekezaji katika kila hatua ya shughuli na mahitaji yao TANESCO, una nafasi kubwa ya kuimarisha ushirikiano na kuongeza ufanisi kwa pande zote mbili.

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages