NEWS

Friday 26 August 2022

TFS yajenga mradi wa maji Chato, Naibu Waziri Masanja auzindua
Na Mara Online News
-----------------------------

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeunga mkono juhudi za kumtua mama ndoo kichwani kwa kujenga mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 22 (pichani juu) katika kijiji cha Butengo wilayani Chato, Geita.

Mradi huo ulizinduliwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja kijijini hapo, jana.

“Mwaka huu kaulimbiu ni kumtua mama ndoo kichwani, hivyo TFS tumeanza kuwatua kinamama ndoo kichwani na tunawatua kwa sababu wamekuwa na mchango mzuri kwenye hifadhi hii,” amesema Naibu Waziri Masanja.

Amewataka viongozi wa kata na vijiji kusimamia vizuri mradi huo ili ulete manufaa yaliyokusudiwa ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji.

“Serikali za vijiji na kata muwe makini katika kusimamia mradi huu kwa kuwa hii ni rasilimali yenu, mkiiharibu ni nyie wenyewe, lakini tunatamani muitunze ili tunapoleta miradi mingine tuone faida za miradi hiyo,” ameongeza.


Naibu Waziri Masanja (kulia) akizindua mradi huo

Aidha, Naibu Waziri huyo amewapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa jitihada kubwa wanazozifanya kulinda Shamba la Miti Silayo, kutunza maeneo ya hifadhi na kuwa na uhusiano mzuri na wahifadhi.

Ametoa rai kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi nchi nzima kuiga mfano wa wakazi wa kijiji cha Butengo kwa kushirikiana na wahifadhi.

“Ninyi mmekuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi na sisi kama Serikali lazima tutimize yale mtakayoyaomba,” amesema Naibu Waziri Masanja.Mbunge wa Chato, Dkt Merdad Kalemani, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kupeleka miradi 11 ya maji katika jimbo hilo, ukiwemo huo uliofadhiliwa na TFS.

Dkt Kalemani amesema uwepo wa mradi huo utapunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Butengo.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Silayo, Juma Mwita, amesema mradi huo unahudumia vitongoji vya Butengo Senta, Butengo na Mwenge vyenye kaya 180 sawa na wastani wa watu 1,080.

Mradi huo umekuwa msaada mkubwa kwa jamii kwa kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji, kwani wanawake wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji.

Pia, umewezesha kupungua kwa magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo safi na salama kama kichocho, kuhara na kipindupindu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages