MBUNGE wa Serengeti, Dkt Amsabi Mrimi (pichani juu aliyesimama), ameiomba Serikali kujenga uwanja wa ndege katika mji wa Mugumu na kuboresha mioundombinu ya barabara, ili kuwezesha wananchi wa jimbo hilo kunufaika na watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Dkt Amsabi ametoa ombi hilo mbele ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alipokuwa katika ziara ya kikazi wilayani Serengeti, Mara hivi karibuni.
“Tunapata watalii wengi lakini hatunufaiki sana kwa sababu hatuna miundombinu,” Dkt Amsabi amemwambia Naibu Waziri huyo.
Mbunge huyo kwa tiketi ya chama tawala - CCM, amesema wananchi wa Serengeti wanakiu ya kujua ni lini ujenzi wa barabara ambazo zimekwama, au ujenzi wake kuchukua muda mrefu utakamilika na hatima ya ujenzi wa uwanja wa ndege katika mji wa Mugumu.
Amesema miundombinu ikiboreshwa itasadia pia kupunguza ukali wa maisha na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika wilaya hiyo ambayo imebarikiwa kuwa na rasilimali ya wanyamapori.
Watalii wakifurahia kutazama makundi ya nyumbu ndani ya Hifadhi ya Tifa ya Serengeti.
Naibu wa Waziri Mhandisi Kasekenya alikuwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa barabara mbalimbali, ikiwemo ya Makutano Juu-Sanzate-Natta.
Ujenzi wa barabara hiyo unaripotiwa kuchukua miaka kadhaa bila kukamilika, licha ya maagizo ya viongozi wa kitaifa kutaka mradi huo ukamilike haraka.
Mhandisi Kasekenya amesema Serikali sasa inataka kujua ni kwanini ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami umegeuka kuwa ‘kichefu kichefu’ kwa muda mrefu.
“Tunataka kujua changamoto nini, ni uwezo mdogo wa mkandarasi, uwezo mdogo wa wafanyakazi, ama kuna changamoto ya vifaa? Tukijua Serikali ichukue hatua, kwa sababu tunataka hii barabara iende [akimaanisha ujenzi wake ukamilike haraka],” amesema.
Amesema Serikali imejipanga kuufungua mkoa wa Mara na kufanya mji wa Mugumu kuwa wa kitalii - akitolea mfano barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo wa Kanda ya Ziwa.
“Lakini sio tu kuufungua mkoa wa Mara, lakini kuunganisha pia na nchi jirani tukijua kwamba moja ya matazamio ni kuufanya mji wa Mugumu kuwa mji muhimu sana kwa ajili ya utalii,” amesema.
Naibu Waziri huyo amesema hata barabara ambazo zilikuwa kwenye mpango, ikiwemo ya Mugumu-Fort Ikoma zitaboreshwa kutokana na umuhimu wake kwa ukuaji wa sekta ya utalii.
Kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege katika mji wa Mugumu, Mhandisi Kasekenya amesema anafahamu kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ina mipango mikubwa kuhusu mradi huo.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment