NEWS

Wednesday 3 August 2022

RMO Mara adaiwa kunyanyasa, kutisha watumishi wake wa afyaNa Mara Online News
---------------------------

MGANGA Mkuu wa Mkoa (RMO) wa Mara, Dkt Juma Mfanga anadaiwa kunyanyasa baadhi ya watumishi wake, wakiwemo wa Hospitali ya Nyamwaga wilayani Tarime.

Pia anadaiwa kutoa vitisho kwa baadhi ya watumishi wa afya katika hospitali hiyo, ikiwemo kuwatishia kuwahamisha kwenda vituo vya kazi nje ya mkoa wa Mara.

Taarifa zilizoifikia Mara Online News leo Agosti 3, 2022 zinaeleza kuwa siku chache zilizopita, Dkt Mfanga alifika katika Hospitali ya Nyamwaga usiku na kuzusha mvutano mkubwa wa mazungumzo na msimamizi wa duka la dawa hospitalini hapo.

Inaelezwa kuwa wakati wa mvutano huo, RMO huyo alimshambulia kwa kumsukuma mtumishi huyo hadi akaanguka na kuumia sehemu ya kichwa.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, baada ya tukio hilo mtumishi huyo alisindikizwa na wenzake kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Nyamwaga ili kupata PF3 kwa ajili ya matibabu.

Taarifa zaidi zinaelezwa kuwa Dkt Mfanga alimuomba msamaha mtumishi huyo akakubali kumsamehe na hivyo suala hilo likaishia hapo kabla ya kuingizwa kwenye kitabu cha malalamiko.

Hata hivyo, inaelezwa kwamba baada ya maafikiano hayo, RMO huyo baadaye aliwafuata baadhi ya watumishi wakiwemo msimamizi huyo wa duka la dawa na mlezi (matron) wa hospitali hiyo na kutoa vitisho, vikiwemo vya kusudio la kuwahamishia nje ya mkoa wa Mara.

Mganga Mkuu huyo wa Mkoa pia analalamikiwa kwamba amekuwa kero na mnyanyasaji wa muda mrefu kwa watumishi wa afya wa halmashauri za mkoani Mara, akidaiwa kutumia madaraka yake vibaya.

“Kwa mfano kuna mtumishi wa kituo cha afya Magoma wilayani Tarime ambaye amelazimika kuacha kazi kutokana na maneno ya kuudhi yakiwemo matusi ya nguoni na vitisho kutoka RMO huyo.

“Sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ziko wazi kuhusu namna ya kumwajibisha mtumishi anapoonekana kufanya kosa, lakini huyo RMO amekuwa akienda kinyume na miongozo hiyo ya Serikali,” kimedokeza chanzo chetu cha habari kwa sharti la kutotajwa jina.

Alipoulizwa na Mara Online News kwa njia ya simu leo Agosti 3, 2022 saa tano asubuhi, Dkt Mfanga amedai kuwa yuko kikaoni na kuahidi kupiga simu baada ya kikao.

Hata hivyo, baada ya Mara Online News kusubiri hadi saa 10 jioni iliamua kumpigia Dkt Mfanga simu tena ambapo iliita bila kupokewa.

Kuona hivyo Mara Online News iliamua kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms), ndipo baadaye akajibu kwa kifupi “Fika ofisini… huyo aliyekutuma mwambie akuwezeshe na nauli”.

Mara Online News inaendelea na juhudi za kutafuta mamlaka zinazohusika na masuala ya haki za watumishi na za binadamu kwa ajili ya kuzungumzia suala la tuhuma hizo zinazoelekezwa kwa RMO huyo.

Juzi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza katika hafla ya kuapisha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wapya, aliwasisitiza viongozi wote wa umma kusimamia sheria, kanuni na taratibu na kuhakikisha haki inatendeka kwa watumishi na wananchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages