Dkt Juma Mfanga
Na Mara Online News
---------------------------
WATUMISHI wa Idara ya Afya katika mikoa ya Mara na Mwanza wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuunda Tume maalum kuchunguza mwenendo wa kiutendaji wa Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) wa Mara, Dkt Juma Mfanga.
Wakizungumza na Mara Online News kupitia simu za mkononi kwa nyakati tofauti juzi na jana, watumishi wa afya kutoka mikoa hiyo walieleza kuchukizwa na tukio la Dkt Mfanga kumshambulia mtumishi wa kike usiku kazini, wakisema ni udhalilishaji wa kijinsia na kinyume na taratibu za utumishi wa umma.
Dkt Mfanga anadaiwa kuwanyanyasa, kuwadhalilisha na kuwashambulia kimwili baadhi ya watumishi wa afya katika maeneo yake ya uongozi.
Baadhi ya watumishi akiwemo wa kituo cha afya Magoma kilichopo wilayani Tarime, inadaiwa wamelazimika kuomba kustaafu na kuacha kazi ili kuondokana na karaha mbalimbali, ikiwemo unyanyasaji wa kisaikolojia kutoka kwa Dkt Mfanga.
“Hujakutana na mkuu wetu [akimaanisha RMO huyo] utatamani unywe sumu ufe,” amesema mmoja wa watumishi hao wakati akizungumza na Mara Online News kwa sharti la kutotajwa jina.
Inadaiwa pia kwamba watumishi wengi walio chini ya RMO huyo hawana amani na molari wa kufanya kazi kutokana na kero wanazopata kutoka kwa daktari huyo.
“Kabla ya kuja hapo mkoani Mara, Dkt Mfanga alikuwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kama DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya. Huku Mwanza alinyanyasa sana Watumishi.
“Cha kushangaza pamoja na unyanyasaji na udhalilishaji wote huo kwa watumishi matokeo yake alipanda cheo na kuwa RMO. Watumishi walijiuliza Serikali ipo wapi?
“Na je, vetting ilifanyika wapi mpaka apate vigezo vya kuteuliwa nafasi ya kuwa RMO. Je mtumishi wa aina hii anastahili kupewa madaraka ya juu wakati ni mnyanyasaji? Ni dhahiri kabisa kuna mtendaji huko juu anamlinda na kumpa madaraka.
"...aliwahi kufanya kitu kibaya sana na cha kinyanyasaji kwa kumpiga mtumishi mmoja wa kike (jina linahifadhiwa) wa zahanati ya Bulale iliyopo jijini Mwanza.
“Tunaomba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Ummy Mwalimu wachunguze juu ya uteuzi huo kwa sababu kiutendaji hafai,” imedai sehemu ya malalamiko ya watumishi wa afya kutoka jijini Mwanza.
Kwa muda mrefu sasa, inadaiwa Dkt Mfanga amekuwa akinyanyasa watumishi wa afya katika halmashauri za mkoa wa Mara na kuwavunja moyo wa kuhudumia wagonjwa.
“Kwa mfano kuna mtumishi wa kituo cha afya Magoma wilayani Tarime ambaye amelazimika kuacha kazi kutokana na maneno ya kuudhi yakiwemo matusi ya nguoni na vitisho kutoka RMO huyo,” amesema mtumishi mwingine wa afya.
Aidha, watumishi hao wameitupia lawama Wizara ya TAMISEMI chini Waziri Innocent Bashungwa, wakidai imeendelea kufumbia macho vitendo vya unyanyasaji dhidi yao.
Mara Online News imeona nakala ya barua ambayo mtumishi huo aliandika kuomba kuacha kazi. Barua hiyo ni ya Mei 2, 2022 ikiwa na kichwa cha habari kinachosema “RESGNATION FROM DUTY AS MEDICAL OFFICER”
Juzi, Mara Online News imepata taarifa kwamba barua ya mtumishi huyo aliyeacha kazi imeombwa ipelekwe ofisi ya Utumishi TAMISEMI, Dodoma.
Watumishi hao wanaamini Tume ya uchunguzi ikiundwa itabaini vitendo vingi vya unyanyasaji vilivyofanywa na Dkt Mfanga dhidi ya watumishi wa afya, kuanzia jijini Mwanza alikokuwa DMO kabla ya kupandishwa kuwa RMO Mkoa wa Mara.
“Maoni ya watumishi wa afya ni kwamba iundwe timu imchunguze Dkt Mfanga maeneo yote aliyopita kufanya kazi ukweli utajulikana kwa sababu hakuna anayemsingizia. Katika vituo vya kazi alivyopita ameumiza wengi sana,” amesisitiza mmoja wa watumishi hao.
Ombi la watumishi hao kutaka iundwe Tume kumchunguza Dkt Mfanga kiutendaji limekuja baada ya Mara Online News kuandika taarifa zinazomtuhumu Dkt Mfanga kushambulia mtumishi wa kike usiku katika Hospitali ya Nyamwaga, wiki iliyopita.
Inadaiwa kwamba Dkt Mfanga alifika katika Hospitali ya Nyamwaga usiku na kuzusha mvutano mkubwa wa mazungumzo na mmoja wa watumishi wa hospitali hiyo.
Inadaiwa wakati wa mvutano huo, RMO huyo alimshambulia kwa kumsukuma mtumishi huyo (jina lipo) hadi akaanguka na kuumia sehemu ya kichwa.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, baada ya shambulio hilo mtumishi huyo alisindikizwa na wenzake kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Nyamwaga ili kupata PF3 kwa ajili ya matibabu.
Taarifa zinadai kuwa Dkt Mfanga alimuomba msamaha mtumishi huyo akakubali kumsamehe na hivyo suala hilo likaishia hapo kabla ya kuingizwa kwenye kitabu cha malalamiko.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa baada ya maafikiano hayo, RMO huyo baadaye aliwafuata baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo na kutoa vitisho, vikiwemo vya kusudio la kuwahamishia nje ya mkoa wa Mara.
Taarifa zaidi kutoka Hospitali ya Nyamwaga zinasema baada ya tukio la kushambuliwa, mtumishi huyo (jina lipo) aliripoti katika kituo cha polisi Nyamwaga kutoa taarifa lakini juhudi zilifanyika kumnusuru RMO huyo dhidi ya kashfa hiyo.
“Tukio lilitokea usiku, akaenda akaripoti polisi, RMO akapigiwa simu lakini hakufika, akaahidi kuwa atakwenda asubuhi. Kesho yake asubuhi alikwenda wakakaa kikao kumuomba asiendelee na kesi mbele ya mabosi wake ambao ni RMO mwenyewe, Kaimu Mganga Mkuu na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Nyamwaga.
“Unategemea angekataa ili kuendelea na kesi mbele ya mabosi wake,” amedokeza mmoja wa watumishi wa hospitali hiyo ambaye ameeleza kuchukizwa na tukio hilo.
Mmoja wa madaktari wa Serikali amesema “Ilitakiwa RMO aweke lock up (rumande) na kuchukuliwa hatua za kisheria. Huu ni ukatili wa kijinisia wa kumshambulia mtumishi tena wa kike akiwa kazini usiku.”
Mbali na kuishia juu kwa juu katika Kituo cha Polisi Nyamwaga, taarifa za tukio hilo ziliripotiwa pia katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari kutoka serikalini.
Wataalamu wa afya wa Serikali wanasema vitendo vya unyanyasaji vikiwemo vya matusi vinavyodaiwa kufanywa na RMO huyo ni hatari kwa utoaji wa huduma bora za matibu katika mkoa wa Mara.
“Ameumiza watu wengi kimwili na kisaikolojia, siyo Tarime tu, hata Musoma Vijijini mpaka ofisini kwake kuna watumishi wanalalamika kunyanyaswana na RMO huyo.
“Mtumishi wa afya akishakuwa “disturbed” anakosa molari ya kuhudumia wagonjwa. Hii ni hatari sana, mamlaka za uteuzi zitazame upya vigezo vya kuwapa watu madaraka ya RMO.
“Kosa la kufanya shambulio la mwili kwa mtumishi mwenzake ni kati ya makosa makubwa yanayoweza kumfukuzisha kazi.
“Hakuna mahali RMO anaruhusiwa kufanya kazi usiku bila kumtaarifu Mkurugenzi na Mganga Mkuu wa Wilaya husika, shambulio alilofanya ni kosa la jinai,” amesema mmoja wa madaktari wandamizi mkoani Mara aliyeomba kutotajwa jina.
Alipoulizwa na Mara Online News kwa njia ya simu Jumatano iliyopita saa tano asubuhi, Dkt Mfanga alidai kuwa alikuwa kikaoni na kuahidi kupiga simu baada ya kikao.
Hata hivyo, baada ya kusubiri hadi saa 10 jioni mwandishi wa habari hizi alimpigia Dkt Mfanga simu tena ambapo iliita bila kupokewa.
Hivyo, aliamua kumtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms), ndipo baadaye akajibu kwa kifupi “Fika ofisini… huyo aliyekutuma mwambie akuwezeshe na nauli”.
Alipotafutwa na Mara Online News kwa njia ya simu ili kuzungumzia suala hilo juzi, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Mara, Benjamin Oganga alisema amepata taarifa za tukio hilo kupitia kwenye chombo cha habari na kuahidi kilitoa ufafanuzi lakini hakufanya hivyo.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt Dorothy Gwajima amesema “Hatua ya kwanza tukio liripotiwe kwenye vyombo vya sheria, kisha vyombo vitasema class, yaani aina ya tukio hilo kama ni ukatili wa kijinsia au aina gani,” Waziri Gwajima ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo mchana.
Waziri Gwajima alikuwa akijibu swali aliloulizwa na Mara Online News la kutaka kujua kauli yake juu ya tukio hilo kama Waziri mwenye dhamana ya kutetea usawa na kupinga ukatili wa kijinsia.
Ameongeza kuwa baada ya tukio hilo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, mawaziri wa kisetka, yaani wa TAMISEMI, Utumishi, Afya na Maenedeleo ya Jamii wanaweza kutoa tamko.
Hata hivyo, Waziri huyo amesisitiza kuwa ukatili hautakiwi kwenye jamii mahali popote pale.
Bado Mara Online News inaendelea na juhudi za kuwapata Mawaziri wenye dhamana, akiwemo Ummy Mwalimu wa Afya na Innocent Bashungwa wa TAMISEMI, kwa ajili ya kuzungumzia suala la tuhuma hizo zinazoelekezwa kwa RMO Mkoa wa Mara, Dkt Mfanga.
Jumatatu iliyopita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza katika hafla ya kuapisha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wapya, aliwasisitiza viongozi wote wa umma kusimamia sheria, kanuni na taratibu na kuhakikisha haki inatendeka kwa watumishi na wananchi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment