NEWS

Thursday 1 September 2022

Gachuma: Mwanza Hotel ni shwari, wateja wanaendelea kupata huduma kama kawaidaChristopher Mwita Gachuma

Na Mara Online News
-----------------------------

MOTO uliozuka kwenye jengo lenye kumbi za harusi, casino na klabu haukugusa New Mwanza Hotel kwani mpaka sasa iko shwari na wateja wanaendelea kupata huduma za malazi, vyakula na vinywaji kama kawaida.

“Jengo letu la hoteli [New Mwanza Hotel] halikuguswa, yaani kwenye upande wa hoteli kila kitu kiko sawa kwa asilimia 100, haina tatizo wala hakuna mgeni aliyepata shida,” mmiliki wa hoteli hiyo, Christopher Mwita Gachuma ameuthibitishia umma kupitia mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Septemba 1, 2022.

Gachuma ametoa ufafanuzi huo kutokana na moto uliosababishwa na shoti ya umeme jana saa mbili usiku katika jengo lake lenye kumbi za harusi, casino na klabu zinazoendeshwa na wapangaji jirani na hoteli hiyo.


Sehemu ya mbele ya New Mwanza Hotel

Ametumia nafasi hiyo pia kutuma shukurani kwa viongozi, taasisi na wananchi wote waliojitokeza kusaidia kudhibiti moto huo.

“Nawashukuru vijana wa zima moto, viongozi wa mkoa na wilaya, bahati nzuri Mkuu wa Mkoa [Adam Malima] aliwahi sana kufika, Mkuu wa Wilaya naye aliwahi sana kufika, kwa hiyo wale viongozi kwa kweli walisaidia sana kuhakikisha kwamba kila kinachotakiwa kinapatikana.

“Watu wengi wametusaidia na nawashukuru wote, wameleta matenki yao ya maji, wafanyabiashara wenzangu, wenye viwanda vya samaki, wanajeshi wametuletea mitambo yao ya zima moto, na wale waliokimbiza magari kutoka Airport (uwanja wa ndege), kwa kweli wamefanya kazi nzuri ambayo ndiyo imesalamisha hali ya hapa.

“Ninawashukuru kwa juhudi zao, wamedhiti moto haukusambaa sana, ungesambaa sana nadhani ungeleta madhara makubwa,” amesema Gachuma.

Hata hivyo, amesema thamani ya hasara iliyosababishwa na moto huo itajulikana baada ya wataalamu husika kufanya tathmini ya vitu vilivyoteketea.

New Mwanza Hotel ni uwekezaji mkubwa wa kifahari unaoendesha huduma zenye hadhi ya kimataifa kwa wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakiwemo watalii wanaotembelea Hifadhi za Taifa za Serengeti, Kisiwa cha Saanane na Kisiwa cha Rubondo - zilizopo Kanda ya Ziwa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages