NEWS

Sunday 18 September 2022

Kewanja FC yatwaa ubingwa Kombe la Mahusiano Barrick North Mara 2022


Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa akikabidhi kombe kwa Timu ya Kewanja FC iliyotwaa ubingwa wa Mashindano ya Soka ya Kombe la Mahusiano 2022 yaliyoandaliwa na Barrick North Mara. Wa pili kutoka kulia ni Menaja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko na Katibu wa Mbunge wa Tarime Vijijini, Remmy Mkapa (kulia).

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
------------------------------------------

TIMU ya Kewanja FC imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Soka ya Kombe la Mahusiano “Mahusiano Cup” baada ya kuichapa Murito FC bao 1-0.

Fainali hiyo ilichezwa kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Ingwe mjini Nyamongo jana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Mgeni rasmi katika fainali hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa alishirikiana na Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko kukabidhi Kewanja FC zawadi za kombe la ubingwa na fedha taslimu Sh milioni 1.5
Wachezaji wa Timu ya Kewanja FC wakifurahia ushindi wa Kombe la Mahusiano 2022 mbele ya viongozi wa Serikali na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.

Murito FC ilipewa zawadi ya Sh milioni moja kwa kuingia fainali na kushika nafasi ya pili katika mashindano hayo ambayo yalishirikisha timu 16 kutoka vijiji mbalimbali vya Halmshauri ya Wilaya ya Tarime.

Vijiji hivyo vilivyoshiriki mashindano hayo ni Genkuru, Msege, Komarera, Nyamwaga, Kewanja, Nyakunguru, Kerende, Nyabichune, Mjini Kati, Matongo, Nyangoto, Mrito, Keisangora na Nyarwana.

Mashindano ya Kombe la Mahusiano yalizinduliwa Septemba 14, mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele kwa kushirikiana na Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko, miongoni mwa viongozi wengine.

Mashindano hayo yaliandaliwa na Kampuni ya Barrick North Mara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, yakiwa na kaulimbiu inayosema “Mahusiano Bora kwa Uwekezaji Endelevu.”
Wachezaji wa timu za Kewanja FC na Murito FC wakimenyana katika mechi ya fainali ya Mashindano ya Kombe la Mahusiano 2022 kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Ingwe mjini Nyamongo.

Kampuni ya Barrick ilitumia mashindano hayo kukuza na kudumisha mahusiano mema kati ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na jamii inayouzunguka.

Aidha, mashindano hayo yatasaidia kuongeza uelewa juu ya fursa mbalimbali zilizopo na kushughulikia masuala mtambuka, hasa uvamizi, uharibifu wa miundombinu (vandalism) na utegeshaji wa mazao, miti na nyumba.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko alisema michezo ni nyenzo muhimu ya katika kujenga na kudumisha mahusiano.

“Bila mahusiano bora sisi kama kampuni hatuwezi kufanya kazi kwa utulivu na jamii inayotuzunguka haiwezi kupata manufaa,” alisema Meneja Lyambiko.

Mkuu wa Wilaya, Kanali Mntenjele aliwataka washiriki wa mashindano hayo kucheza kwa amani na wasimamizi husika kutenda haki bila kupendelea timu yoyote.

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara aliipongeza Barrick North Mara kwa kuandaa mashindano hayo, akisema yatahamasisha ushirikiano kutoka kwa jamii inayozunguka mgodi huo ili kuwezesha kila upande kunufaika.

Uzinduzi wa mashindano ya soka ya Mahusiano Cup pia ulitanguliwa na michezo mbalimbali ikiwemo ya kuvuta kamba, kufukuza kuku na ngoma ya asili, kabla ya timu za Kewanja FC na Mosege FC kucheza mechi ya ufunguzi.

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages