
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, akizungumza na wananchi katika kata ya Kigunga wakati wa ziara yake wilayani Rorya, Agosti 14, 2026.
Tarime, Rorya
---------------------
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amekemea vitendo vya uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, akisema vina madhara makubwa kwa uchumi na maendeleo ya taifa.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika wilaya ya Rorya inayopakana na ziwa hilo mkoani Mara, Agosti 14, 2026, Waziri Bashiru aliwataka wananchi kushirikiana na serikali kukomesha vitendo hivyo kwa manufaa ya jamii na taifa.
"Uchumi wa Rorya najua unategemea kilimo, uvuvi na ufugaji. Mitego inayovua inaua samaki wadogo na mayai yake, samaki wanaopatikana ni wachanga - hawana ladha,” alisema.
Kuhusu samaki aina ya sato, alisema serikali imeamua kuzuia kuingiza samaki hao kutoka nje ya nchi ili kulinda wavuvi, usalama na masoko ya Tanzania.
Kwa upande mwingine, alikagua miundombinu ya Mnada wa Mifugo Randa na kituo cha utafiti na uzalishaji wa vifaranga vya samaki cha TAFIRI kilichopo Sota – Shirati.

Waziri Bashiru (aliyevaa kaunda suti) na msafara wake akikagua bwawa la ufugaji wa samaki Shirati
Awali, Waziri Bashiri akiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, alikagua na kuzindua miradi mbalimbali, ikiwemo ya majengo ya huduma za mama na mtoto, kichomea taka cha kisasa na vyumba vya kuhifadhia maiti iliyotekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 900.
Aliwapongeza wasimamizi wa utekelezaji wa miradi hiyo akisema "Mmetekeleza miradi kwa kuzingatia thamani ya fedha, hata kwa macho inaonekana bila utaalamu.”

Waziri Bashiru (katikati mbele) akiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele (kushoto), kukagua miradi ya Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime.
No comments:
Post a Comment