NEWS

Thursday, 15 September 2022

Udanganyifu wadaiwa kugubika kinyang’anyiro cha Uenyekiti UVCCM Wilaya ya Tarime, baadhi ya watia nia wadaiwa kughushi vyeti




Na Mara Online News
----------------------------------

KINYANG’ANYIRO cha nafasi ya Uenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, kinadaiwa kugubikwa na udanganyifu kutokana na baadhi ya watia nia kudaiwa kughushi vyeti vya kuzaliwa.

Mara Online News imedokezwa kuwa umri wa baadhi ya watia nia wa nafasi hiyo unatofautiana katika vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya Taifa [NIDA].

“Kuna mwanachama ana umri wa miaka zaidi ya 30, lakini cheti chake cha kuzaliwa alichoambatanisha na fomu yake ya kutia nia kinaonesha umri wake hauzidi miaka hiyo, lakini pia baadhi ya watia nia wamepandikizwa kwa maslahi ya watu binafsi,” kimedai kimojawapo cha vyanzo vyetu vya habari kutoka ndani ya CCM.

Inadaiwa watia nia hao wameghushi vyeti vya kuzaliwa ili kutimiza sharti la umri usiozidi miaka 30 unaohitajika kugombea nafasi ya Uenyekiti wa UVCCM Wilaya.

Siku chache zilizopita, Katibu Mkuu wa UVCCM, Kenani Kihongosi alikaririwa na vyombo vya habari akiwataka watendaji husika ngazi ya wilaya na mkoa nchini, kuhakikisha umri wa kila mgombea wa nafasi ya uongozi ndani ya Umoja huo hauzidi miaka 30, ili kutoa fursa ya uongozi kwa vijana katika chama hicho tawala.

Mara Online News inaendelea na juhudi za kuwapata wasemaji wa Chama hicho kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages