NEWS

Wednesday 21 September 2022

WWF yazindua mradi wa uhifadhi wa ardhi oevu ya MaraNa Mara Online News
------------------------------

SHIRIKA la Kimataifa la Uhifadhi wa Maji na Mazingira (WWF) Tanzania, limezindua mradi wa miaka mitatu wa uhifadhi wa ardhi oevu ya Mara.

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika mjini Musoma, Septemba 19, 2022 na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali, mgeni rasmi akiwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Msalika Makungu aliyewataka washiriki kuwa mabalozi wa kuhamasisha uhifadhi wa eneo hilo, kwani ni makazi muhimu ya samaki na viumbe kimbizi.

“Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuchangia kwa mawazo na vitendo katika kulinda eneo hili,” amesisitiza Makungu (katikati pichani juu).

Wadau walioshiriki katika uzinduzi huo ni viongozi na wawakilishi wa Vitengo vya Usimamizi wa Mialo (BMUs), Jumuia za Watumia Maji, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dakio la Mara, Shirika la Wakulima na Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria (VIFAFIO), maafisa kilimo na uvuvi, miongoni mwa wengine.


Akiwasilisha mada katika uzinduzi huo, Mratibu wa Programu ya WWF Tanzania, Christian Chonya amesema mradi huo utahusisha vijiji 27 vyenye watu zaidi ya 110,000.

Chonya amesema mradi huo utatekelezwa ili kukabiliana na vitendo vya uharibifu wa ardhi oevu ya Mara na uvuvi usiyo endelevu, ukiwemo wa kutumia nyavu haramu - unaochangia kudhoofisha eneo hilo na kuathiri upatikanaji wa samaki.

“Kupungua kwa samaki katika eneo hili kumekuwa kichocheo cha kuwekwa mipango na mikakati ya kuhakikisha viumbe hawa wanalindwa na pia maisha ya watu wanaotegemea ardhi hii yanakuwa bora zaidi,” amesema.

Chonya akiwasilisha mada wakati wa uzinduzi wa mradi huo

Kwa mujibu wa Chonya, mradi huo unafadhiliwa na Idara ya Mazingira, Chakula na Maendeleo ya Jamii ya Uingerez (DEFRA), kupitia mradi wake w Darwin Initiative.

Ametaja malengo ya mradi huo kuwa ni kuchapisha utafiti wa kwanza wa hali halisi ya samaki na kusaidia mpango shirikishi wa menejimenti ya uvuvi na kupunguza hatari kwa baioanuai kwenye kilomita za mraba 192.


Malengo mengine ni kuhamasisha uvuvi endelevu utakaosaidia kupunguza uvuvi haramu kwa asilimia 60, kuwezesha fursa ya kujipatia kipato kwa wanawake na kusaidia watu 1,250 katika vijiji vya mradi ili kuboresha maisha yao na hali zao za kiuchumi, amesema.

Kulingana na Chonya, utekelezaji wa mradi huo utahusisha shughuli za kukusanya taarifa za awali na kutengeneza mfumo bora wa ufuatiliaji na usimamizi wa uvuvi, hususan kupitia takwimu zilizopo, kuandaa utafiti juu ya masoko na uchumi ili kuelewa tabia, hali za maisha na utawala katika maeneo ya uvuvi.


Shughuli nyingine ni kujenga uwezo wa kuwezesha uvuvi endelevu na utekelezaji wa mpango shirikishi kupitia mafunzo kwa viongozi sita wa vitengo vya usimamizi wa uvuvi vya kijamii watakaokuwa mabalozi wa uvuvi endelevu na kufundisha wanajamii 510 kuhusu uvuvi huo, matumizi ya zana bora za uvuvi, sayansi ya jamii na usimamizi.

Pia kupitia na kuboresha mipango mbalimbali ya serikali za mitaa na wilaya ili kujumuisha mafunzo na matokeo ya mradi, kubainisha/ kutambua fursa ya kifedha kusaidia usimamizi shirikishi wa uvuvi na kubadilishana uzoefu na wataalamu wa uvuvi wa kitaifa na kimataifa.


Kwa upande wao, wadau mbalimbali wamelipongeza Shirika la WWF wakisema mbli na kusaidia kulinda usalama wa samaki katika eneo oevu la Mto Mara na Ziwa Victoria linalopokea maji ya mto huo, mradi huo utakuwa na manufaa makubwa ya kiafya, kimazingira na kiuchumi kwa jamii.

Akizungumza na Mara Online News muda mfupi baada ya uzinduzi wa mradi wa uhifadhi wa ardhi oevu ya Mara, Mtafiti kutoka TAFIRI, Joseph Luomba amesema taasisi hiyo imejipanga kushirikiana na WWF na wadau wengine ili kufikia malengo ya mradi huo.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo na Uvuvi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Revocatus Lutunda amesema uhifadhi wa ardhi oevu ya Maraa ni muhimu kwa ajili ya kuzuia uchafu mbalimbali usiingie Ziwa Victoria na kuathiri viumbe waliomo.

“Kwa maana nyingine ni kwamba mradi huu unakwenda kulinda maji ya Ziwa Victoria na samaki waliomo pamoja na viumbe wengine. Lakini pia uhifadhi wa eneo hilo utalifanya kuwa kivutio cha utalii,” amesema Lutunda.


Mkurugenzi wa VIFAFIO, Majura Maingu naye amelipongeza Shirika la WWF kwa kubuni mradi huo, akisema umezingatia mahitaji ya kijamii na kiuchumi na kukumbusha wananchi wajibu wa kulinda uhai wa eneo oevu la Mara.

“Sehemu kubwa ya eneo hili limeathirika kutokana na shughuli za binadamu zikiwemo za kilimo, ufugaji na uvuvi usiyo endelevu. Hivyo mradi huu utaunganisha nguvu ya wadau mbalimbali katika kulihifadhi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo,” amesema Maingu

Naye Afisa Maji Dakio la Mara, Mwita Mataro amesema mradi huo utawezesha ardhi oevu ya Mara kutangazwa rasmi kuwa hifadhi maalumu itakayotambulika na kulindwa kisheria.

Mataro akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo

Ardhi oevu ya Mara yenye ukubwa wa kilomita za mraba 387 inayopatikana mkoani Mara, Tanzania na kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria, ni miongoni mwa ardhi oevu kubwa zaidi katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ardhi oevu hiyo inatajwa kuwa ni eneo lenye baioanuai muhimu kidunia na hutoa huduma mbalimbali za kiikolojia, ikiwemo uvuvi ambao ni muhimu zaidi kwa vijiji 27 vyenye watu zaidi ya 110,000.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages