Na Mara Online News
------------------------------
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mara imeendesha semina ya kuelimisha na kujulisha wafanyabiashara wa wilayani Tarime (pichani juu) mabadiliko ya sheria za kodi yaliyofnywa na Bunge na kuanza kutumika rasmi Julai 1, 2022.
Semina hiyo imeendeshwa na Afisa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Mkoa wa Mara, Geofrey Comoro mjini Tarime, jana Septemba 20, 2022.
Kwa mujibu wa Comoro, mabadiliko hayo ya sheria za kodi yamewalenga wafanyabiashara wadodo na wa kati wenye mauzo yasiyozidi shilingi milioni 100.
Amefafanua kuwa mfanyabiashara mwenye mauzo yasiyozidi shilingi milioni nne anayetunza na asiyetunza kumbukumbu hatatozwa kodi, na mwenye mauzo yanayoanzia shilingi milioni nne hadi saba anatakiwa kulipa kodi kiasi cha shilingi laki moja.
“Mfanyabiashara mwenye mauzo yanayoanzia shilingi milioni saba hadi yasiyozidi milioni 11 kodi yake itakuwa shilingi laki mbili na nusu na mwenye mauzo kuanzia shilingi milioni 11 mpaka yasiyozidi milioni 100 atatozwa asilimia 3.5,” amesema Comoro.
Afisa huyo wa TRA amesema lengo la mabadiliko hayo ya kikodi ni kukuza uchumi katika sekta ya usafirishaji na kuleta maisha bora kwa wananchi.
Comoro akiwasilisha mada katika semina hiyo. (Picha zote na Mara Online News)
Akizungumza na Mara Online News muda mfupi baada ya semina hiyo, msafirishaji wa mizigo kutoka forodha ya Sirari kwenda mikoa mbalimbali ya Tanzania, David Mbondi amesema semina hiyo imemwezesha kuelewa mabadiliko ya viwngo vya kodi.
“Tunaishukuru TRA kwa sababu semina hii imetuwezesha kuelewa mabadiliko ya sheria za kodi na viwango vyake na tumehamasishwa kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa letu. Pia tunaishukuru Serikali yetu chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio cha wananchi na kurekebisha tozo mbalimbali,” amesema Mbondi.
Aidha, Mbondi ametoa wito kwa wafanyabiashara wote kuwa na wazalendo kwa taifa lao kwa kuhakikisha wanalipa kodi na kwa wakati.
“Tusikwepe kulipa kodi, maana kukwepa kodi ni kujidanganya, leo unakwepa kodi kesho unahitaji barabara, leo unakwepa kodi kesho unahitaji madawa hospitalini. Kodi imerekebishwa niwaombe wafanyabiashara wenzangu tulipe kodi, kodi ni msingi wa maendeleo kwa taifa letu,” amesisitiza Mbondi.
Katika hatua nyingine, maafisa wa TRA imekutana na Klabu ya Kodi ya Shule ya Sekondari ya Katulu wilayani Rorya na kupokea wanachama wapya wa klabu hiyo, Ijumaa iliyopita.
Comoro amesema baada ya mapokezi hayo waliwapa wanachama wapya na wa zamani elimu juu ya masuala mbalimbali ya kodi ili kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa TRA wa masuala ya kodi katika familia na jamii zao.
No comments:
Post a Comment