NEWS

Tuesday 4 October 2022

Mkurugenzi Professor Mwera Foundation awatangazia wahitimu kidato cha IV ofa maalumu



Na Mara Online News
-------------------------------

MKURUGENZI wa Taaisisi ya Professor Mwera Foundation (PMF), Hezbon Peter Mwera (pichani juu aliyesimama), ametoa ofa maalumu ya mafunzo ya ufundi kwa wanafunzi wanaoelekea kuhitmu kidato cha nne katika shule zote za sekondari zilizopo Halmshauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara.

“Tutawapatia mafunzo ya ufundi bure na kila mmoja atachagua aina ya mafunzo anayopenda katika Chuo cha Mafunzo ya Fundi Tarime,” Hezbon ambaye pia ni Mkuu wa Chuo hicho alisema, wiki iliyopita.

Alitangaza ofa hiyo katika mahafali ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari ya Wasichana (Tarime Girls Secondary School) ya mwaka huu. Shule hiyo ipo nje kidogo ya mji wa Tarime.

“Hii ofa ni kwa wanafunzi watakaohitimu katika shule yetu ya Tarime Girls na itaenda sambamba kwa wanafunzi wote watakaomaliza kidato cha nne katika shule zilizopo Halmashauri ya Mji wa Tarime kupitia mpango wa kusadia vijana wa Tarime,” alisema Hezbon ambaye pia hivi karibuni alichaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa.

Wahitimu wa kidato cha nne Tarime Girls wakiwa wamemvisha mlezi (matron) wao zawadi ya kitenge.

Shule ya Tarime Girls na Chuo cha Ufundi vinamilikiwa na Taasisi ya PMF ambayo mwasisi wake ni Prof Peter Mwera, mmoja wa wawekezaji wazawa mkoani Mara, ambao wanatajwa kuwa na mchango mkubwa katika kutoa ajira na kusaidia kuboresha huduma kwa jamii.

Aidha, Hezbon alitumia fursa hiyo kutangaza mpango wa kuifanya Tarime Girls kuwa ya mchanganyiko kuanzia mwakani, ili iwe na fursa ya elimu ya sekodari kwa wavulana pia.

“Tunataka kuifanya shule hii ianze pia kuchukua wavulana na maandalizi yanaendelea vizuri, hata majengo muhimu yamekamilika,” alisema

Alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wazazi kuiifanya shule hiyo na chuo chake dada cha ufundi kuwa chaguo kwa vijana wao kupata elimu na mafunzo bora ya ufundi.

Hezbon alisema Taasisi ya PMF imeendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu na mafunzo ya ufundi kwa vijana ili kuwandaa kuwa na mchango muhimu kwa maendeleo ya jamii na taifa.

Wanafunzi wa Tarime Girls wakionesha sehemu ya mafunzo kwa vitendo wanayopata shuleni hapo.

Katika hatua nyingine, mdau wa maendeleo ya sekta ya elimu, Nyambari Nyangweine ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Tarime, aliahidi kutoa msaada wa vitabu vyenye thamani ya shilingi milioni tatu katika shule hiyo ya Tarime Girls.

Ahadi hiyo iliwasilishwa katika mahafali hayo na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Sauti ya Mara, Jacob Mugini, ambaye alikuwa Mgeni rasmi.

“Mheshimiwa Nyambari Nyangwine ambaye ni mdau wa elimu na mpenda maendeleo amenituma niwape salamu na kuahidi kuipatia hii vitabu vyenye thamani shilingi milioni tatu,” Mugini alisema katika sehumu ya hotuba yake.

Mugini pia ambaye ni Mkurugenzi wa Mara Online, alikabidhi msaada wa mipira ya miguu minne katika shule hiyo wakati wa mahafali hiyo.

“Sisi kama Mara Online tunatoa msaada wa mipira minne ya kisasa ili kusaidia maendeleo ya michezo ya shule ya Tarime Girls,” alisema.

Mgeni rasmi, Jacob Mugini akimkabidhi mwanafunzi Maria Kahindi [mmoja wa wahitimu wa kidato cha nne Trime Girls] cheti cha kufanya vizuri katika somo la Kiingereza.

Mugini alitumia nafasi hiyo pia kuwataka wahitimu hao kuendelea kusoma kwa bidii ili waweze kufikia ndoto zao za elimu.

“Kusoma shule binafsi (private school) ni bahati kwenu, hongereni kwa hatua hii na ni matarajio ya kila mtu hapa kuwa wote mtapata darala la kwanza katika mtihani wenu wa kitaifa,” Mugini ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, aliwambia wahitimu hao.

Aliwataka pia kudumisha nidhamu na kujiepusha na vikundi au kujihusisha na vitendo ambavyo vinaweza kukatisha ndoto zao za elimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Tarime, Maria Daniel Tarimo, alisema shule hiyo imeweka mikakati ya kuondoa daraja sifuri kwa kila somo na kuwatabiria wahitimu hao kufanya vizuri katika mtihani wao wa kumaliza kidato cha nne.

“Kwa miaka mitatu mfululizo shule yetu imekuwa ikishika nafasi ya kwanza kiwilaya katika mitihani ya kitaifa ya kidato cha pili kwa kufaulisiha kwa asilimia 100 na kwa matokeo ya kidato cha nne cha mwaka 2019 shule yetu iliongoza kwa kushika nafasi ya kwanza, mwaka 2020 ilikuwa miongoni mwa shule tatu zilizokuwa na matokeo mazuri katika wilaya ya Tarime,” alisema Maria.

Ofisa wa TAKUKURU (kushoto) akimkabidhi Mwalimu wa Tarime Girls vyeti kwa ajili ya kuwatunuku wanafunzi wa shule hiyo waliofanya vizuri katika utoaji wa elimu ya kupiga vita rushwa.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya PMF, Mchungaji Paul Baru ambaye ni Askofu wa Huduma wa Yesu Tumaini Kuu (Jesus Great Hope) aliwataka wahitimu hao kuendelea kuzingatia maadili mema na kumtegemea Mungu hata watakapokuwa nje ya shule.

Mchungaji Baru alisema Taaisi ya PMF inaunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kutokomeza maadui watano ambao ni maradhi, ujinga, umaskini, rushwa na ufisadi.

“Ni muhimu kwa wadau wote kuwa na nguvu ya pamoja kupinga maadui hawa watano kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema kiongozi huyo wa kiroho.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages