NEWS

Monday 3 October 2022

Naibu Waziri Sagini azindua ujenzi wa ofisi ya RPC Tarime-RoryaNa Mara Online News
------------------------------

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini (pichani juu kulia), leo Oktoba 3, 2022 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya.

Katika hotuba yake wakati wa uzinduzi huo mjini Tarime, Sagini ambaye pia ni Mbunge wa Butiama mkoani Mara, ameeleza kuridhishwa na hatua ya ujenzi huo.


Hata hivyo, amelitaka Jeshi la Polisi kuboresha mazingira ya eneo la ofisi hiyo, kwa kupanda miti ya kivuli, matunda, maua na mapambo.

Aidha, amelipongeza Jeshi la Polisi Tarime-Rorya kwa kazi nzuri ya kulinda usalama wa raia na mali zao, huku akilitaka kutofumbia macho mtu yeyote atakayetishia usalama na amani kwa wananchi.

Naye Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Lucas Mkondya aliyemwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini katika uzinduzi huo, amesema kuanzishwa kwa Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya kumesaidia kupunguza uhalifu unaovuka mipaka.

“Kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kuendelea kulinda mafanikio yaliyofikiwa [na Jeshi la Polisi] ili wananchi waendelee kupata fursa ya kufanya shughuli za kujiletea maendeleo,” amesema DCP Mkondya.

Amesema Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya ulianzishwa Julai 9, 2009 kutokana na vitendo vya wizi wa mifugo, ujambazi wa kutumia silaha na mapigano ya koo za kabila la Wakurya vilivyokuwa vimekithiri.


Awali, Kamanda wa Polisi Tarime-Rorya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Geofrey Sarakikya (wa tatu kushoto waliokaa), amemueleza Naibu Waziri Sagini kwamba ujenzi wa jengo la ofisi hiyo ulianza Oktoba 23, 2021 na hadi sasa umefikia asilimia 97.

ACP Sarakikya amesema ujenzi wa ofisi hiyo umegharimu shilingi bilioni 1.5 zilizotolewa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, na kwamba ikikamilika italiondolea jeshi hilo adha ya kupanga kwenye majengo ya taasisi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages