NEWS

Sunday 16 October 2022

SIKU YA CHAKULA DUNIANI: Barrick yapeleka msaada wa vyakula kwenye vituo vya kulea watoto TarimeNa Mwandishi Wetu, Tarime
---------------------------------------

KAMPUNI ya Barrick North Mara imeadhimisha Siku ya Chakula Duniani, kwa kupeleka msaada wa vyakula mbalimbali kwenye vituo viwili vinavyolea watoto takriban 200, waliotoka mazingira magumu wilayani Tarime.

Vituo hivyo ni City of Hope kilichopo kijiji cha Ntagacha na Angel House Children’s Home cha kijijini Gamasara, nje kidogo ya mji wa Tarime mkoani Mara.

“Leo [jana] ni Siku ya Chakula Duniani na sisi Barrick North Mara tumefurahi kusherekea siku hii kwa kutoa msaada wa vyakula kwa ajili ya watoto waliotoka mazingira magumu wanaolelewa kwenye vituo viwili viwili,” Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Gilbert Mworia alisema wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vyakula hivyo katika vituo hivyo, jana.

Baadhi ya vyakula hivyo ni mchele, maharage, sukari, unga mahindi, ngano, mafuta ya kupikia, mbuzi, chumvi na sabuni za unga.

“Katika Barrick tunasema hakuna mtu anatakiwa kupata njaa na ndio maana sisi kama wadau tumetumia Siku hii ya Chakula Duniani kuonesha mfano wa juhudi zetu katika kuhakikisha hakuna mtu anakosa chakula,” alisisitiza Mworia.

Mlezi wa kituo cha Angel House, Anna Migera Chacha aliishukuru Kampuni ya Barrick, akisema msaada huo una umuhimu mkubwa kwa watoto wanaolelewa kituoni hapo.

“Mpaka sasa kituo chetu kina watoto 73 ambao wanasoma kuanzia chekechea hadi chuo kikuu, hivyo watafurahia kupata chakula kizuri. Tunamshukuru Mungu kwa msaada huu, tunawashukuru sana Barrick na wabarikiwe kwa kutuletea msaada huu,” alisema Anna.


Usalama wa chakula ni moja ya maeneo matano ambayo Kampuni ya Barrick inayapa kipaumbele katika mpango wake wa maendeleo endelevu kwa jamii zinazoishi jirani na migodi yake wa North Mara uliopo Nyamongo, Tarime.

Maeneo mengine yanayopewa kipaumbele katika kampuni hiyo ni elimu, maji, afya na uchumi.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni Barrick kwa bia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Kampuni ya Barrick imekuwa ikitenga mabilioni ya fedha kugharimia miradi ya kijamii katika vijiji vilivyo jirani na mgodi wa North Mara tangu mwaka 2019, kupitia Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages