Na Mwandishi Wetu, Rorya
-----------------------------------------
MKURUGENZI wa Professor Mwera Foundation (PMF), Hezbon Peter Mwera (katikati pichani juu), ametoa misaada mbalimbali kuchangia utatuzi wa changamoto zinazoikabili Shule ya Sekondari ya Kutwa Kirogo iliyopo wilayani Rorya.
Michango hiyo ni mbao zenye thamani ya shilingi milioni moja, mchele kilo 100 kwa ajili ya chakula cha watahiniwa siku ya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne, mipira mitatu ya michezo, mapipa mawili ya kuhifadhia maji kwenye vyoo vya wanafunzi na kugharimia utapishaji wa choo chao.
Hezbon ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya wahitimu wa kidato cha nne shuleni hapo wiki iliyopita, aliwahamasisha watahimiwa kujiandaa vizuri kuelekea mtihani wao wa taifa utakaofanyika Novemba mwaka huu.
Aliwapa mbinu mbalimbali za maandalizi ya kufanya vizuri katika mtihani huo, ikiwa ni pamoja na kurudia masomo waliyofanya, kutatua maswali na kufanya mijadala kwenye vikundi.
Hezbon Peter Mwera (katikati waliosimama mwenye suti ya kaki) katika picha ya pamoja na walimu, wanafunzi na viongozi mbalimbali wakati wa mahafali hayo.
Mkurugenzi huyo wa Taasisi ya PMF ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, alitumia nafasi hiyo pia kuhamasisha wazazi na wadau wengine kuchangia maendeleo ya shule hiyo, ambapo aliongoza harambee ndogo iliyofanikisha upatikanaji wa Sh 950,000.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kirogo, Mwalimu Elisha Andrew alimshukuru Hezbon, wazazi na wadau wengine, alisema misaada hiyo itasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, ikiwemo utengenezaji wa viti na meza kwa ajili ya wanafunzi na walimu.
Kwa mujibu wa Mwalimu Elisha, kwa sasa shule ina wanafunzi 204 wa kidato cha kwanza hadi cha nne, wakiwemo wavulana 110 na wasichana 94.
Aidha, alibainisha kuwa wanafunzi wa kidato cha nne wanaoelekea kufanya mtihani wa kuhitimu ni 52 - kati ya 180 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2019. Wengine 128 hawapo kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo za mimba na maradhi.
Chanzo: Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment