NEWS

Monday 10 October 2022

Waziri Aweso: MUWASA kwa sasa mko vizuri sana


Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kushoto) akifurahia zawadi ya picha yake iliyochorwa - aliyopewa na MUWASA wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Tisa ya Mamlaka hiyo mjini Musoma, juzi. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Meja Jenerali (Mstaafu) Joseph Michael aliyemkabidhi zawadi hiyo.

Na Mwandishi Wetu, Musoma
-----------------------------------------

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Jambo ambalo nataka niliseme kutoka kwa dhati ya moyo wangu, MUWASA kwa sasa mpo vizuri sana,” Waziri Aweso alisema katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bodi ya Tisa ya MUWASA mjini Musoma, juzi.

Aweso alisema hali ya utendaji katika mamlaka hiyo ilikuwa mbaya miaka kadhaa iliyopita.

“Miaka ya nyuma hapa [MUWASA] kulikuwa hakuna nidhamu, itoshe tu kusema nimefurahi sana. Mimi nawaombea dua muendelee kufanya vizuri,” aliongeza waziri huyo.

Alieleze kutambua na kuthamini kazi nzuri iliyofanywa na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, CPA Joyce Msiru, kabla ya kumteua kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira katika Wizara ya Maji.

“Nimpongeze sana Joyce. Joyce alifanya kazi nzuri sana katika mamlaka hii,” Waziri Aweso alisema na kutaja baadhi ya miradi ya maji iliyosimamiwa na MUWASA, ukiwemo uhuishaji huduma ya maji ya bomba katika mji mdogo wa Shirati wilayani Rorya na ujenzi wa chujio la maji bwawa la Manchira, Mugumu wilayani Serengeti.

Waziri Aweso alimpongeza pia Mkurugenzi Mtendaji wa sasa wa MUWASA, Mhandis Nicas Mugisha na watumishi wote kwa utendaji kazi mzuri na utayari wa kuendelea kuleta mageuzi makubwa katika mamlaka hiyo, ambayo mtandao wake wa majisafi na salama umefikia asilimia 95 ya wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.

“Nicas anafanya kazi nzuri, ameiheshimisha mmlaka hii. Ninakushukuru sana sana Nicas na watumishi wote wa MUWASA. Watumishi wana morali kubwa endeleeni kupacha kazi, Musoma sasa mambo ni bam bam,” alisema.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (wa tatu kutoka kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Nicas Mugisha (wa kwanza kushoto) na viongozi wengine wakifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Tisa ya Mamlaka hiyo mjini Musoma, juzi.

Aliipongeza pia kazi nzuri iliyofanywa na Bodi ya Nane ya MUWASA na kuitaka Bodi ya Tisa kuendeleza juhudi hizo.

“Mwenyekiti wa Bodi nikupongeze sana, Bodi ya Nane imefanya kazi kubwa na nzuri, na nina imani Bodi ya Tisa itafanya kazi mzuri kwa umoja na mshikamno,” alisema.

Bodi ya Tisa ya MUWASA inaendelea chini ya Uenyekiti wa Meja Jenerali (mstaafu) Joseph Michael Isamuhyo aliyeteuliwa kwa mara nyingine kuongoza bodi hiyo.

Aweso aliahidi ushirikiano kwa Bodi hiyo na menejimenti ya MUWASA, ili kuiwezesha mamlaka hiyo kufikia malengo yake.

Sambamba na hilo, Waziri Aweso aliahidi kufanyia kazi ombi la shilingi bilioni mbili lililotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Mhandisi Nicas Mugisha, kwa ajili ya kugharimia uwekaji wa mabomba mapya ya maji katika mji wa Musoma.

Kuhusu maslahi ya watumishi wa MUWASA, Waziri Aweso alielekeza yaangaliwe, stahiki zao zilipwe kwa wakati na kupewa motisha.

“Maslahi ya wafanyakazi wenu ni jambo la msingi sana. Msikilize changamoto za wafanyakazi na kuzitatua,” alisisitiza, huku akiwataka nao kuwa na kauli nzuri kwa wateja.

Aliagiaza pia Bodi ya MUWASA kusimamia ulinzi na utunzaji wa yanzo vya maji na kudhibiti upotevu wa maji yanayozalishwa na mamlaka hiyo ambayo chanzo chake kikubwa ni Ziwa Victoria.

Katika hotuba yake hiyo, Waziri Aweso aliagiza pia bodi hiyo kuawandoa watu wote waliovamia vyanzo vya maji, kwa faida ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Majukumu mengine ambayo Waziri huyo alitaka yasimamiwe na bodi hiyo ni pamoja na kushughulikia malalamiko ya wateja kwa wakati na kusimamia mapato na matumizi ya mamlaka hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya MUWASA alimhakikishia Waziri Aweso kuwa watasimimamia na kutekeleza maelekezo hayo, huku akioa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea kuipatia mamlaka hiyo mamilioni ya fedha kugharimia utekelezaji wa miradi ya maji.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (katikati waliokaa), Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Mhandisi Nicas Mugisha (kushoto waliosimama), viongozi wengine na wajumbe wa Bodi ya Tisa ya Mamlaka hiyo katika picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo mjini Musoma, juzi.

“Kama bodi, tunakuomba utufikishie pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais [Samia Suluhu Hassan] kwa pesa anazotupatia, tunashukuru sana,” alisema Meja Jenerali Isamuhyo.

Aidha, bodi hiyo ilimpogeza Aweso ikisema anafanya kazi nzuri ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani.

“…Wewe [Aweso] ni mmoja wa mawaziri wachapa kazi,” alisema Mwenyekiti huyo wa Bodi ya MUWASA.

Mafanikio ya MUWASA
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Mhandisi Nicas Mugisha, alisema mamlaka hiyo imefanikiwa kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia zaidi ya 50 hadi asilimia 38.

Mhandisi Mugisha alisema MUWASA pia imeweza kuongeza mapato yake kutoka Sh milioni 248.7 mwaka 2018 hadi milioni zidi ya 300 kufikia mwaka 2021.

Mafanikio mengine ya MUWASA, ni kuongeza mtando wa maji ya bomba kutoka urefu wa kilomita 277 hadi kilomita 382 na kupunguza uchakavu wa mabomba kwa asilimia 9.8.

Mhandisi Mugisha aliongeza alitaja mafanikio mengine ambayo mamlaka hiyo imeyapata kuwa ni kulipa malimbikizo ya madeni ya watumishi, kupata hati safi na kuunganisha baadhi ya wananchi na Benki ya Equity kwa ajili ya kupewa mikopo ya kuunganishiwa huduma ya maji ya bomba.

Kikundi cha Kwaya ya Wizara ya Maji kikitumbuiza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Tisa ya MUWASA, iliyohutubiwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara mjini Musoma, juzi. (Picha zote na Sauti ya Mara)

Salamu za RC Mara
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt Halfan Haule alisema katika mwaka wa feddha uliopita, Wizara ya Maji ilitoa Sh bilioni 19 ambazo ziligharimia utekelezaji wa miradi maji 91 ya maji mkoani hapa, ikiwemo inayosimamiwa na RUWASA, jambo ambalo limengeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo aliipongeza MUWASA, akisema ni moja ya taasisi za Serikali zinazotekeleza ilani ya chama tawala - CCM kwa vitendo katika Manispaa ya Musoma.

Mathayo alitumia nafasi hiyo pia kukazia ombi la shilingi bilioni mbili lililotolewa na MUWASA kwa Waziri Aweso, akisema zitawezesha mamlaka hiyo kutandaza mabomba mapya katika mji wa Musoma.

“Nakuomba Mheshimiwaa Waziri kamalize haka kakero ka bilioni mbili,” Mbunge huyo alimuomba Waziri Aweso.

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages