NEWS

Thursday 6 October 2022

Wizara ya Maji yatoa maelekezo kwa wahasibu wake



Na Mwandishi Wetu, Mwanza
-------------------------------------------------

WIZARA ya Maji imewalekeza wahasibu wa sekta ya maji kufanyia kazi maeneo yenye changamoto, ikiwemo ufungaji wa hesabu za mwisho na mikataba, ili kuepusha kujirudia kwa hoja za kiukaguzi.

Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Maji, CPA Ahadi Msangi (pichani juu aliyesimama) ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga, ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wahasibu wa sekta ya maji jijini Mwanza, leo Oktoba 6, 2022.

CPA Msangi amewakumbusha wahasibu hao jukumu lao la msingi la kuweka mifumo ya udhibiti (internal control), ili kupunguza hoja za ukaguzi na uwezekano wa kusababisha hasara kwa Serikali na utendaji usioridhisha.

“Katika usimamizi wa fedha yapo maeneo ya kuboresha kutokana na hoja zinazotoka kila mwaka - kuna nyingine zinajirudia; natumaini kutokana na kikao hiki mtakuja na maboresho ama maazimio kwenye maeneo ya mahesabu na mikataba ambayo kila mwaka yanajitokeza,” ameelekeza.

Ametaja majukumu makubwa ya wahasibu kuwa ni pamoja na kuhakikisha mali za umma zinatumika kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu, miongozo na ushauri wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali.


“Ikumbukwe kwamba ni wajibu wa wahasibu kuhakikisha taarifa zinaandaliwa kwa viwango vya kimataifa na kusimamia masuala yote ya mali na fedha za Serikali na kushauri masuala yote yanayohusiana na usimamizi wa fedha,” ameelekeza CPA Msangi kwa niaba ya Katibu Mkuu.

Aidha, amewakumbusha wahasibu wote wa sekta ya maji kuzingatia maadili ya taaluma zao; ambayo ni pamoja na kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na weledi.

Awali, akizungumza kabla ya ufunguzi rasmi wa kikao hicho, Mwenyekiti wa Wahasibu wa Mamlaka za Maji nchini, CPA Leonard Chale ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Maji Dodoma, amesema lengo la kukutana kwao ni kupata uelekeo wa pamoja kwa wahasibu wote walio chini ya Wizara ya Maji.

“Tumekutana hapa kubadilishana uzoefu, kujengeana uwezo kulingana na hali halisi ya kazi zetu, kujadili changamoto tunazokutana nazo na kupata ufumbuzi wa pamoja,” amesema CPA Chale.

Amebainisha kuwa kikao kazi hicho ni maelekezo ya Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), aliyotoa kwa watumishi wote wa sekta ya maji - kuhakikisha kila kada inakutana kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja, kwa maenedeleo ya sekta hiyo.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kinafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) - maarufu kwa jina la Maji House, kuanzia Oktoba 6 hadi 7, 2022, kikiwashirikisha wahasibu kutoka Wizara ya Maji Makao Makuu, Mamlaka za Maji, Ofisi za Mabonde, Chuo cha Maji, RUWASA na Mfuko wa Maji nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages