NEWS

Wednesday, 17 June 2026

Waziri Aweso aipiga chini Menejimenti ya MWAUWASA kwa 'kumzingua'



Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (nyuma ya aliyevaa kofia), akiongozwa na Menejimenti ya MWAUWASA kukagua miundombinu ya maji jijini Mwanza jana.

Na Mwandishi Wetu
Mwanza
--------------

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameivunja Menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kufuatia kutoridhishwa kwake na kiwango cha utoaji huduma ya majisafi na salama jijini Mwanza.

Uamuzi huo umefuatia ziara ya kikazi aliyoifanya jijini Mwanza, ambapo amebaini uwepo wa changamoto za upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi, changamoto ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na udhaifu wa kiutendaji.

Akizungumza na watumishi wa MWAUWASA jana, Waziri Aweso, alisema kwamba licha ya mamlaka hiyo kuwa miongoni mwa taasisi bora za maji nchini, utendaji wake wa sasa hauendani na matarajio ya serikali na wananchi.

“Kwa sasa siridhishwi na utendaji wa MWAUWASA na ninyi wenyewe mmekiri. Asilimia kubwa ya changamoto nilizobaini kwenye ziara yangu ni za kiutendaji,” Waziri Aweso alisema.

Aliongeza kuwa amekuwa akitoa maelekezo mara kwa mara kwa Menejimenti ya MWAUWASA kuhusu umuhimu wa uwajibikaji na kuongeza ufanisi, lakini hakuna mabadiliko aliyoyaona.

“Naivunja Menejimenti ya MWAUWASA na kuanza upya. Tutatengeneza timu mpya ya watendaji kwa dhumuni la kuimarisha utendaji na kuongeza ufanisi wa taasisi hii muhimu,” alisisitiza.

Waziri Aweso alifafanua kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha menejimenti mpya itakayoundwa itawajibika kikamilifu katika kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa Mwanza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, alisema wizara hiyo haitasita kuchukua hatua dhidi ya watumishi wasiowajibika katika maeneo yote nchini.

“Wizara itaendelea kufuatilia utendaji kwa karibu. Nawasisitiza watumishi wa MWAUWASA kubadilika, kwani uwajibikaji wenu ndio utakaopunguza changamoto zinazowakabili wananchi,” alisema Mhandisi Mwajuma.

Waziri Aweso amekuwa akiwaonya watendaji wababaishaji katika sekta ya maji akisema "Ukinizingua, tunazinguana".

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages