NEWS

Tuesday 22 November 2022

AICT Mara, Right to Play wahamasisha elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu Tarime Vijijini


Afisa Elimu Kata ya Nyansincha, Mwl Sophia Range (katikati) na Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota wakikabidhi kombe kwa washindi wakati wa tamasha la michezo la kuhamasisha elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu, lililofanyika Shule ya Msingi Iramba katika kijiji cha Kangariani wilayani Tarime, hivi karibuni. (Picha na Ernest Makanya)

Na Mwandishi Wetu, Tarime
-------------------------------------------

KANISA la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Right to Play, wametumia tamasha la michezo ya wanafunzi wilayani Tarime, kuhamasisha jamii kutowabagua watoto wenye mahitaji maalumu, hasa wenye ulemavu katika suala la elimu.

Akizungumza wakati wa tamasha hilo lililofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Iramba katika kijiji cha Kangariani kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara hivi karibuni, Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota alisema mradi huo unalenga kuleta usawa na haki katika jamii.

“Mradi huu unalenga kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu kufikiwa na elimu ili iwe msaada kwao. Kaulimbiu ya mradi huu inasema ‘Ondoa Vikwazo, Jenga Jamii Bora na Jumuishi Inayofikika kwa Wote,” alisema Rebeca.

Alifafanua kuwa watoto wenye ulemavu wakipata elimu itawasaidia kuondokana na utegemezi na hali ya kuwa mzigo katika familia na jamii kwa ujumla.

“Vile vile elimu kwa watoto wenye ulemavu itasaidia kuondoa ile dhana kuwa mlemavu hana msaada kwenye familia na kwamba ulemavu ni laana katika jamii,” aliongeza.

Naye mgeni rasmi katika tamasha hilo, Mwalimu Sophia Range ambaye ni Afisa Elimu Kata ya Nyansicha, alisema kuna faida nyingi kuwapa watoto wenye mahitaji maalumu elimu na iliyo jumuishi.

Mwalimu Sophia alizitaja faida hizo kuwa ni pamoja na kuifanya jamii kupiga hatua kimaendeleo.

“Kuruhusu watoto na watu wote wenye ulemavu kuchangamana na wasio na ulemavu kutawanjengea uwezo mkubwa wa kufanya kazi,” alisema.

Mgeni rasmi huyo alitumia nafasi hiyo pia kushukuru na kupongeza Shirika la Right to Play na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kujali na kuhamasisha elimu bora na jumuishi kwa watoto wenye mahitaji maalumu katika jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages