NEWS

Monday 7 November 2022

Serikali yatoa tamko kuhusu wanaodai fidia ya maduara NyamongoNaibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa akizungumza kikaoni.

Na Mwandishi Wetu, Tarime
------------------------------------------

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imewataka watu wanaodai fidia ya maduara ya uchimbaji dhahabu na mali nyingine zilizokuwa kwenye eneo la Nyabigena lililochukuliwa na mwekezaji wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kuwasilisha vielelezo.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa alitoa agizo hilo wakati akihitimisha kikao chake na wawakilishi na viongozi wa wananchi hao mjini Tarime jana, ambapo aliwataka kuwasilisha vielelezo kwa Afisa Madini wa Mkoa wa Mara kufikia Novemba 30, mwaka huu.

"Nimepokea taarifa za kutatanisha juu ya mikataba yenu na mwekezaji… Hatuwezi kufikia muafaka bila vielelezo, na vielelezo hivyo viwe na ushahidi kwamba wewe ndiye ulikuwa mmiliki wa shimo na makubaliano mliyoingia yanasemaje,” alisema Dkt Kiruswa.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo wa Madini ambaye alisema ametumwa na Rais wa Jamhuri ya Muungno wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutatua mgogoro huo, alimtaka kila mdai kusimamia ukweli - akitahadharisha kuwa bila vielelezo sahihi, madai hayatafanyiwa kazi.

Alifafanua kuwa Serikali inahitaji kupata vielelezo vya mkataba wa kila kijiji kuhusu madai ili wadai halali haweze kulipwa haki zao.

“Ninatoa muda wa kuwasilisha vielelezo hadi tarehe 30 mwezi huu [Novemba], mkishindwa kutekeleza haya maagizo nitanawa mikono,” alisema Dkt Kisurwa na kuiagiza ofisi ya madini mkoa wa Mara kuendelea kuelimisha viongozi na wananchi wa eneo hilo sheria na taratibu za uchimbaji madini.

Aidha, Dkt Kisurwa aliuagiza uongozi wa Barrick North Mara kuandaa mikataba waliyorithi kutoka kwa watangulizi wake na namna walivyoifanyia kazi ili isaidie kupata suluhisho la mgogoro uliodumu miaka mingi.

“Lengo ni kubaini madai halali, walengwa na kuamua anayestahili kulipa. Rais wetu [Samia Suluhu Hassan] anataka haki, wewe ukidandia haki isiyo yako hautalipwa,” alisema.

Kwa upande wake, Afisa Madini wa Mkoa wa Mara, Joseph Martin alisema ofisi yake imebaini udanganyifu katika madai ya wananchi hao na kushauri sheria ichukue mkondo wake dhidi ya wahusika.

“Kuna mtu amezaliwa mwaka 1996 lakini anadai fidia, tukabaini janjanja, ushauri wangu sheria ifuatwe, madai yana ujanja. Kwa mujibu wa sheria iliyokuwepo, wengi walikuwa wamepangishwa na watu wenye ardhi walilipwa fidia, tumebaini hawana nyaraka (documents) ya madai yao,” alisema Martin.

Nao wabunge Mwita Waitara wa Tarime Vijijini na Agnes Mathew (Viti Maalum Mkoa wa Mara) walitangaza katika kikao hicho kwamba hawako tayari kutetea waongo katika mgogoro huo.

Mbunge Waitara alisema angetamani kuona migogoro mingi inayosonga mgodi huo inapungua ili washughulikie masuala ya maendeleo ya wananchi.

“Mgodi upo ‘stranded’, na wanatushangaa sisi ndio tanakwamisha kuendeleza uwekezaji. Wenye haki mtapata, watu wote waongo hao mimi sio wenzangu,” alisisitiza Waitara.

Naye Mbunge Agnes aliunga mkono msimamo wa Waitara wa kukataa wanaosema uongo kwenye madai hayo.

“Wawekezaji ni neema, sio laana, mimi pia naungana na Mheshimiwa Waitara kukataa waongo katika suala hili,” alisema Mbunge Agnes.

Baadhi ya wananchi hao walimueleza Naibu Waziri Kisurwa kuwa hawadai asilimia, bali ni fidia ya maduara na mali nyingine zikiwemo nyumba na vifaa vya uchimbaji vilivyohabiribiwa na mwekezaji wa mgodi wa North Mara baada ya kukabidhiwa eneo hilo.

Lakini katika hali ya kushangaza wananchi hao walitumia fursa hiyo ‘kuvuana nguo’ mbele ya Naibu Waziri Kisurwa, wakilaumiana wenyewe kuhusu idadi halisi ya watu wanaodai fidia, ambapo baadhi walidai ni 77 na wengine walisema ni 362.

Mgogoro uliopo unahusisha wadai 362 wa fidia ya mashimo ya uchimbaji dhahabu katika eneo la Nyabigena lililobinafsishwa na Serikali kwa mwekezaji wa mgodi wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime miaka ya 1990.

Taarifa zilizowasilishwa na baadhi ya viongozi wa wadai hao mbele ya Naibu Waziri Kisurwa, zinaeleza kuwa vijiji vitano vilikabidhi mashimo hayo kwa watu wenye uwezo wa kuyaendesha kabla ya kufunga mkataba wa kuyakabidhi kwa mwekezaji wa wakati huo, Kampuni ya Afrika Mashariki Gold Mine.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko alimweleza Naibu Waziri Kisurwa katika kikao hicho kuwa mkataba waliomiliki kwa mwekezaji mtangulizi wa Kampuni ya Barrick mgodini hapo unatambua vijiji vitano na siyo mtu mmoja mmoja.

“Natambua kuwa kuna mkataba wa vijiji vitano zinavyostahili kuwa vinapata asilimia moja,” alisema Lyambiko akivitaja vijiji hivyo kuwa ni Nyangoto, Kewanja, Kerende, Nyamwaga na Genkuru, ambavyo mkataba unaonesha viliingia makubaliano na mwekezaji ya kulipwa asilimia moja ya uzalishaji wa dhahabu katika mgodi huo.

Hata hivyo, alisema uchimbaji ulisimama katika eneo la Nyabigena tangu mwaka 2012, lakini akadokeza kuwa unaweza kuanza tena ili kuwezesha wanavijiji kuendelea kupata matunda ya asilimia moja, ikiwa changamoto zilizopo ikiwemo kesi ya utwaaji wa ardhi itatatuliwa.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa sasa unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kuputia Kampuni ya Twiga Minerals.

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages