NEWS

Monday, 21 November 2022

TARURA kuleta mageuzi ya miundombinu ya barabara Serengeti


Ujenzi wa barabara inayosimamiwa na TARURA ukiendelea katika barabara ya Nyichoka-Maburi wilayani Serengeti, hivi karibuni.

Na Mwandishi Maalumu, Serengeti
---------------------------------------------------

FEDHA za matengenezo ya barabara zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika Wilaya ya Serengeti mkoni Mara zimeongezeka kutoka Sh milioni 890 hadi bilioni 2.39 kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Serengeti, Mhandisi Michael Alphonce, ongezeko hilo limetokana na fedha za tozo ya mafuta - kiasi cha Sh bilioni moja na Sh milioni 500 za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo zinazotolewa na Serikali.

Hata hivyo Mhandisi Alphonce anasema pamoja na ongezeko hilo, bado mahitaji ni makubwa katika wilaya hiyo yenye mtandao wa barabara zenye urefu wa kilomita 971.78.

“Mahitaji ni makubwa, tukipata bilioni mbili zaidi zitatusaidia kupunguza changamoto zilizopo, lakini bado tunajitahidi na kuhakikisha kuwa barabara zinapitika,” amesema Mhandisi huyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili wilayani hapa, juzi.

Anasema fedha zinazotolewa na Serikali hutumika kugharimia matengenezo mbalimbali ya barabara zilizo chini ya TARURA katika wilaya hiyo yenye utajiri mkubwa wa wanyamapori.

“Hali ya barabara za huku Serengeti ilikuwa mbaya zaidi wakati tulipokuwa tunapata shilingi milioni 890, lakini sasa hivi tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muunagno wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa sababu fedha ya tozo imetuongezea nguvu.

“Kwa sasa tunapiga hatua na kuna mabadiliko makubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma tuliyokuwa tukipokea shilingi milioni 890,” anasema Mhandisi Alphonce.

Anasema sehemu kubwa ya fedha hizo zimeelekezwa kwenye ukarabati na ufunguzi wa barabara muhimu, zikiwemo zinazowezesha wananchi kufikia huduma za Kijamii,kiuchumi na kiusalama.

“Kuna barabara zilizokuwa hazipitiki na muhimu kwa huduma za kijamii kama vile shule, masoko, zahanati, vituo vya afya na ofisi za serikali za vijiji.

“Pia kulikuwa na shida ya wananchi kufikia mnada wa Kinoko, hasa mvua ilipokuwa ikinyesha watu walikuwa hawapiti, barabara zote hizo tumezitenegeza na sasa zinapitika,” anaongeza.

Mwaka 2021/2022
Kaimu Meneja huyo wa TARURA Serengeti, anaeleza kuwa katika mwaka wa fedha uliopita [2021/2022], TARURA Serengeti ilitumia fedha za tozo ya mafuta kufanikisha matengenezo mbalimbali ya barabara.

Anazitaja barabara hizo kuwa ni Kwitete-Msongo wa Gete (km 9), Masangura (km 7), Kenyana-Gantamome (km 7.5) na Morotonga-Mbilikili (km 6).

Anafafanua kuwa matengenezo ya barabara hizo yalihusisha kazi za kunyanyua matuta, kumwaga changarawe, kujenga makaravati na mitaro ya kuongoza maji.

Kuhusu malalamiko yaliyotolewa na madiwani wa Halmshauri ya Wilaya ya Serengeti kwamba barabara nyingi katika halmashauri hiyo hazipitiki kwa urahisi na zimegeuka kuwa mahandaki, Mhandisi Alphonce anasema marekebisho na maboresho yanaendelea kufanyika kwenye mtandao wa barabara zilizo chini ya TARURA.

Wakizungumza kwa hisia kali katika kikao cha baraza lao mjini Mugumu hivi karibuni, madiwani wengi walidai kuwa robo tatu ya barabara zilizo chini ya TARURA katika halmashauri hiyo zimegeuka kuwa mahandaki na hazipitiki kwa urahisi.

Sh bilioni moja
Hata hivyo kupitia Sh bilioni moja za tozo ya mafuta mwaka huu wa fedha [2022/2023], TARURA inaendelea kufanya matengenezo na maboresho mbalimbali katika barabara za wilayani Serengeti, ikiwemo ya Stendi Mpya-Koreri katika kata ya Matare ambapo tayari mkandarasi amepelekwa kujenga eneo lililobomolewa na maji ya mvua.

“Sehemu inayosumbua katika kata ya Matare ni ya mita 800 na mkandarasi tayari yupo site (eneo la kazi) na kazi iko mbioni kukamilika.

“Siyo Matare tu, wakandarasi wako site na matengenezo yanaendelea kwenye barabara mbalimbali,” anasema Mhandisi Alphonce.

Anazitaja barabara zilizo kwenye mpango wa kufanyiwa matengenezo ya kunyanyua matuta, kumwaga changarawe, kujenga makaravati na mitaro ya kuongoza maji kwa sasa kuwa ni pamoja na Maburi-Nyichoka yenye urefu wa kilomita sita.

“Matengenezo ya Barabara hii yatakuwa na manufaa kwa wananchi ambao wamekuwa wakishindwa kupita kwenda soko la Monuna,” anasema.

Barabara nyingine zinazotengenezwa ni Issenye-Wagete-Rigicha (km 4.5), Tabora B-Kibeyo (km 3), Mugumu-Masangura-Kemgesi (km 3), Nyamburi-Tamkeri-Mbalibali (km 3), Shule ya Msingi Metemo (km 6) na Daraja Mbili-Sogoti (km 3).

Sh milioni 890
Kwa upande mwingine, barabara kadhaa wilayani Serengeti zinafanyiwa mtengenezo mbalimbali kutokana na Sh milioni 890 za matengenezo ya kwaida mwaka huu.

Barabara hizo ni Kemgongo-Nyamatoke (km 2.5), Msati-Mara Somoche (km 2), Gentamome-Borenga (km 9), Shule ya Sekondari ya Maji Moto (km 1.7), Ryoba (km 0.77), Kadogoo (km .17) na Setco (0.5).

Nyingine zinzofanyiwa matengenezo ni Nginga (km 0.24), Mhegete (km 0.86), Morotonga (km 0.41), Nyamohanga (km 0.38), Manao (km 0.5), Sokoine na Magufuli.

Pia barabara ya Manchira (km 3.8) imo kwenye mpango wa kutengenezwa. “Barabara hii italimwa ili iweze kupitika kwa urahisi maana imekuwa changamoto kwa wananchi,” Mhandisi Alphonce anasema.

Sh milioni 500
Kulingana na Kaimu Meneja huyo wa TARURA Wilaya ya Serengeti, Sh milioni 500 na Serikali kupitia Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo kwa sasa zimeelekezwa kugharimia matengenezo ya barabara za lami katika mji wa Mugumu.

“Kwa sasa wilaya ya Serengeti ina barabara za lami zenye urefu wa kilomita 4.2. Matengenezo tunayofanya kwenye barabara hizi ni pamoja na kusafisha mitaro na kuziba maeneo yaliyotoboka,” anafafanua.

Mhandisi Alphonce anasema bila Sh bilioni moja za tozo ya mafuta na milion 500 za Mfuko wa Jimbo zinazotolewa na Serikali, hali ya barabara katika wilaya ya Serengeti ingekuwa mbaya.

“Mahitaji [ya matengenezo ya barabara] katika wilaya yetu ya Serengeti ni makubwa kuliko bajeti. Tukiongezewa shilingi bilioni mbili zitasaidia kupunguza changamoto zilizopo,” anasisitiza.

Hata hivyo mhandisi huyo anaweka wazi kuwa ufinyu wa bajeti ya barabara katika wilaya ya Serengeti unatokana na idadi ndogo ya wakazi wake.

“Unajua Serengeti ina eneo kubwa la utawala ila idadi ya watu ni ndogo ukilinganisha na maeneo mengine,” anasema.

Mhandisi Alphonce anatumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuwataka wafugaji kuacha kupitisha mifugo katikati ya barabara kwa kuwa vitendo hivyo vinaharibu miundombinu hiyo na kusababisha adha kwa wananchi.

“Tunawaomba madiwani wasaidie kuhimiza wananchi kulinda barabara na hifadhi zake, TARURA tuko pamoja nao, sisi ni taasisi sikivu,” anasema Mhandisi Alphonce.

Sehemu ya barabara ya Kwitete-Mosongo-Wegete iliyofanyiwa matengenezo na TARURA wilayani Serengeti, hivi karibuni.

Meneja wa TARURA Mkoa wa Mara, Mhandisi Boniface William anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya miundombinu ya barabara zilizo chini ya TARURA katika wilaya ya Serengeti na wilaya zingine za mkoa wa Mara.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutuongezea bajeti ya kwa ajili ya matengenezo ya barabara zetu kutoka shilingi bilioni 6.9 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 hadi shilingi bilioni 25 kwa mwaka huu wa fedha unaoendelea [2022/2023],” anasema Mhandisi William.

Anawahakikishia wananchi wa wilayani Serengeti kuwa mtandao wa barabara zilizo chini ya TARURA utaendelea kuboreshwa

“Tunawaomba wananchi wa Serengeti waendelee kuiamini TARURA na tupo kwa ajli ya kuhakikisha barabara zao zinapitaka kwa urahisi na kazi inaendelea,” anasema Mhandisi William.

Meneja huyo wa TARURA Mkoa wa Mara anasisitiza pia umuhimu wa wananchi wa mkoa huo kuendelea kutunza miundombiu ya barabara.

“Lazima kila mwananchi aone umuhimu wa kutunza miundombinu ya barabara kwani Serikali inawekeza fedha nyingi sana kwenye matengenezo ya barabara,” anasema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma anasema matarajio yake sasa baada ya TARURA kuongezewa bajeti hiyo, ni kuona matengenezo na maboresho ya barabara nayo yanaongezeka katika wilaya hiyo inayopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Ninaishukuru Serikali kuongeza fedha za barabara na ninaiomba iendelee kuongeza zaidi bajeti hiyo ili kukidhi mahitaji ya matengenezo ya barabara za wilaya yetu ya Serengeti,” anasema Makuruma ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Busawe.

Naye Mbunge wa Serengeti, Amsabi Mrimi anaishukuru Serikali akisema “Ninaamini pamoja na kwamba bado ongezeko hilo la fedha za barabara zetu halikidhi mahitaji makubwa tuliyonayo, barabara zinazolengwa zitatengenezwa kwa ubora unaoridhisha.”

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages