NEWS

Monday 14 November 2022

Wapigaji wa fedha za umma Bunda wanalindwa na nani?



Na Mwandishi Wetu
-----------------------------

HIVI karibuni, Mbunge wa Bunda Vijijini, Boniphace Mwita Getere alizungumza kwa hisia kali Bungeni Dodoma, akilalamikia ‘upigaji’ wa kutisha wa fedha za umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Alikwenda mbali zaidi na kumuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amteue kuwa Waziri wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI hata kwa siku moja, ili akomeshe ‘madudu ya upigaji’ wa fedha za miradi ya umma yanayoendelea katika halmashauri hiyo na maeneo mengine nchini.

“Hivi hizi hela za umma zitaliwa mpaka lini? Hivi mimi, si nimuombe Mama [akimaanisha Rais Samia] aniteue hata Waziri wa TAMISEMI jamani hata siku moja? Aah, hivi tunafanyaje sasa? Hivi tunafanyaje vitu vinaliwa vinaenda - vinaliwa, vinaliwa tunaangalia kwanini?” Getere alihoji.

Mbunge huyo aliinyooshea kidole Halmashauri yake ya Wilaya ya Bunda akidai imekithiri kwa hujuma na matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii.

Alitolea mfano fedha alizoziita mbichi - kiasi cha milioni 96 ambazo alidai ‘zililiwa’ kabla hazijaingia benki, huku shilingi milioni 626 zilizotolewa na Rais Samia kugharimia ujenzi wa jengo la halmashauri hiyo zikiwa zimeelekezwa kwa wazabuni waliochelewesha kazi.

Malalamiko ya ubadhirifu wa fedha za umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda yamekuwa ya muda mrefu sasa. Wananchi na viongozi wao wanalalamika lakini ni kama hawasikilizwi na mamlaka za juu serikalini.

Cha kushangaza zaidi ni kwamba vitendo vya ‘ulaji’ na matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi katika halmashauri hiyo vimeendelea kuwepo licha ya malalamiko yanayotolewa.

Miradi ya elimu na afya miongoni mwa mingine inatekelezwa chini ya kiwango na kucheleweshwa kutokana na ubadhirifu wa fedha husika.

Maswali makuu matatu yanatosha kujiuliza: Nani anawalinda wezi, wafujaji, wabadhirifu na wahujumu wa fedha za umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda? Anawalinda kwa maslahi ya nani? Na ni kweli kwamba huyo anayewalinda yuko juu ya sheria?

Ni wazi kwamba watendaji wa Serikali katika halmashauri hiyo hawawezi kukwepa tuhuma hizo na wanastahili kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria, kwa manufaa ya umma wa wana-Bunda na Taifa kwa ujumla.

Kuna haja ya mamlaka za juu serikalini kufunguka katika haya yanayoendelea ndani ya Halmashauri hiyo, ziwamulike kwa jicho kali wabadhirifu wa fedha za umma waliokita huko, ikiwa ni pamoja na kupeleka timu maalum ya uchunguzi na kuwafikisha mahakamani kwa hatua za kisheria.

Hatua hizo ni muhimu kuchukuliwa haraka kwa sababu inaleta taswira mbaya kusikia kwamba watu wachache wanaendelea kuhujumu na kuiba fedha za Serikali kipindi hiki ambacho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anajizatiti kutafuta fedha kwa wahisani nje ya nchi kwa ajili ya kuboreshea wananchi huduma za kijamii.

Ni aibu kubwa kuendelea kuwafumbia macho watumishi wanaohujumu maendeleo ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Taifa kwa kujineemesha binafsi na fedha zinazotolewa na Serikali kugharimia miradi ya huduma mbalimbali za kijamii.

Sitaki kuamini kwamba wasaidizi wa Mhe. Rais Samia wameshindwa kumsaidia kwa kuchukua hatua za makusudi kukomesha ‘upigaji’ unaoelekea kuota mizizi ndani ya halmashauri hiyo iliyopo mkoa wa Mara alikozaliwa Rais wa Kwanza na Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Msisitizo ubaki pale pale kwamba wabadhirifu wa fedha za umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda wasifumbiwe macho, wachukuliwe hatua kali bila huruma kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hilo ndilo litakuwa suluhisho na jibu la kumridhisha hata Mbunge Getere aliyehoji bungeni kwa hisia kali: “Tunamhurumia nani anayekula fedha za umma? Kwanini watumishi wa Serikali wa Tanzania hawaogopi hela ya umma? Wanaokula hela ni walewale - wanaokula hela ni walewale tu. Kuna nini kinaendelea hapa [Bunda]?”

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages