Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (kushoto) akikabidhi Tuzo ya Mlipa Bora kwa Meneja wa Barrick nchini Tanzania wa Fedha na Utawala, Melkiory Ngido (katikati) katika hafla ya Mlipakodi ya TRA iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja wa Kodi wa Twiga, Judith Chambua.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
-------------------------------------------------
MGODI wa Twiga Minerals wa North Mara, umeshinda Tuzo ya mshindi wa kwanza ya Mlipakodi Bora katika hafla ya mwaka huu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kutoa tuzo kwa walipa kodi bora nchini.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.
Twiga Minerals Corporation, inasimamia shughuli za: Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu mkoani Shinyanga; Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Tarime - pamoja na Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi (Pangea) ambao pia upo Shinyanga na kwa sasa upo katika hali ya kufungwa.
Mwaka wa 2020, Twiga Minerals Corporation ililipa kodi ya mapato kiasi cha dola milioni 119, ambapo mwaka 2021, ililipa dola milioni 96.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Habari Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye na Watendaji Waandamizi wa TRA na Wizara ya Fedha katika picha ya pamoja na Watendaji kutoka taasisi mbalimbali zilizoshinda Tuzo ya Mlipa Kodi Bora 2022.
Mapema mwaka huu, Wizara ya Madini iliitambua Twiga kama mchangiaji mkubwa wa mapato ya Serikali kwa mwaka 2021. Kampuni yake tanzu - North Mara Gold Mine pia ilishinda tuzo ya Mshindi wa Kwanza miongoni mwa Wamiliki wa Leseni Maalumu za Uchimbaji katika Utekelezaji sera ya ushirikishwaji wazawa katika mnyororo wa uchumi wa madini (Local content) kwa mujibu wa Sheria ya Madini kifungu namba 123 mnamo mwaka 2021.
Akitoa taarifa ya utendaji wa kampuni katika kipindi cha robo mwaka kwa vyombo vya habari Oktoba mwaka huu, Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Barrick Gold Corporation, Dkt Mark Bristow alisema Twiga imechangia kwa dola zaidi ya bilioni 2.187 katika uchumi tangu mwaka 2019. Kati ya hizo, dola milioni 878 zililipwa katika mfumo wa ushuru na kodi mbalimbali za Serikali.
Kuhusiana na kusaidia ukuzaji wa biashara za ndani, Dkt Bristow alisema asilimia 80 ya manunuzi ya kampuni yenye thamani ya kiasi cha dola bilioni 1.025 yalikuwa ya bidhaa za ndani.
No comments:
Post a Comment