NEWS

Wednesday, 18 March 2026

Watoto zaidi ya 800,000 kupewa chanjo ya polio mkoani Mara



Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Zabron Masatu akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari mjini Musoma jana kuhusu ujio wa chanjo ya ugonjwa wa polio kwa watoto wenye umri wa kuanzia miaka 10 kushuka chini. (Na Mpigapicha Wetu)

Na Mwandishi Wetu
Musoma
-----------------

Watoto zaidi ya 832,448 wanatarajiwa kupewa chanjo ya ugonjwa wa polio (kupooza) kwa watoto wote wenye umri wa kuanzia miaka 10 kushuka chini mkoani Mara.

Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO) wa Mara, Dkt. Zabron Masatu, aliyasema hayo jana mjini Musoma wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa waandishi wa habari kuhusu masuala ya chanjo hiyo.

Dkt. Masatu ambaye pia ni Kaimu Katibu wa Mkoa wa Mara, alisema utoaji wa chanjo hiyo utatolewa kuanzia Machi 24 hadi 27, 2026 nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha kuwa watoto wote wanafikiwa kwa urahisi.

Alisema mbali na mkoa wa Mara, alisema mpango wa utoaji wa chanjo hiyo utatekelezwa pia katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Tabora na Singida.

“Chanjo hii itatolewa nyumba kwa nyumba na kwenye maeneo yenye mikusanyiko kama vile shuleni, ibadani na masokoni,” Dkt. Masatu na kusisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kushiriki kikamilifu katika kuelimisha jamii kuhusu faida za chanjo hiyo.

Lengo la chanjo hiyo ni kuwakinga watoto hao dhidi ya virusi vya polio, ingawa Dkt. Masatu alisema kwamba kwa mara ya mwisho kesi ya mtu mwenye virusi hivyo Tanzania iliripotiwa Julai 1996.

Alibainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imeamua kutoa chanjo hiyo kwa watoto hao kipindi hiki baada ya virusi vya polio kugundulika kwenye majitaka katika mkoa wa Mwanza mwaka jana.

Hivyo, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbambali imeamua kuchukua tadhari kutoa chanjo hiyo katika mkoa wa Mwanza na mikoa jirani.

Dkt. Masatu aliwaomba waandishi wa habari kutumia taaluma yao kuhamasisha wananchi kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa wahudumu wa afya watakaopita kutoa chanjo hiyo ili kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa huo.

Alieleza kuwa chanjo ya polio ni salama na yenye ufanisi mkubwa katika kuzuia ulemavu wa kudumu na hata vifo vinavyoweza kusababishwa na ugonjwa hatari wa polio.

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, anatarajiwa kuzindua utoaji wa chanjo hiyo Machi 24, mwaka huu mkoani Mwanza.

Dkt. Masatu alisema chanjo ya polio ni salama na akatoa wito kwa wazazi/ walezi kutoa ushirkiano wa kuruhusu watoto wao kupewa kinga hiyo ddhidi ya ugonjwa huo hatari.

“Watoto wote walio chini ya miaka 10 na hata ambao walishapatiwa chanjo hii watachanjwa tena, haina madhara - badala yake inawaongezea kinga zaidi,” alifafanua Dkt. Masatu.

Naye Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Mara, Flowina Muuzaje, alisisitiza kuwa huduma ya chanjo hiyo itatolewa kwenye makazi ya watu na maeneo mengine ya mikusanyika kama vile shuleni, nyumba za ibada na masoko.

Kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali za kuhakikisha kuwa ugonjwa wa polio (kupooza) unatokomezwa kabisa Tanzania.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt. Zabron Masatu (katikati waliokaa) ambaye pia ni Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, Mugini Jacob (kulia waliokaa), wakiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari waliopatiwa mafunzo ya uelewa kuhusu chanjo ya Polio, mjini Musoma jana.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages