NEWS

Monday 19 December 2022

DC Tarime akemea 'uhuni' unaofanywa na watu waliolipwa fidia ili kumpisha mwekezaji Barrick North Mara eneo la Komarera


Na Mara Online News
-------------------------------------

MKUU wa Wilaya (DC) ya Tarime mkoani Mara, Kanali Michael Mntenjele (pichani), amesema kinachofanywa na baadhi ya watu waliokwishalipwa fidia ya mali zao ili kupisha upanuzi wa shughuli za mwekezaji wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara katika eneo la Komarera ni uhuni.

Kanali Mntenjele ametoa kauli hiyo katika mahojiano na vyombo vya Mara Online News na Sauti ya Mara ofisini kwake mapema leo Desemba 20, 2022. Alikuwa akitoa ufafanuzi juu ya video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii jana ikionesha ubomoaji majengo katika eneo la Komarera.

“Kinachofanyika ni uhuni fulani kwa sababu watu walishafanyiwa tathmini na Serikali, na tathimini ile ilifanywa kwenye vitu vilivyokuwepo kabla ya katazo au zuio la kuendeleza yale maeneo.

“Kwa hiyo tathmini ilifanyika, wamekwishalipwa, huyo mwenyewe aliyetuma hiyo clip amekwishalipwa milioni 78 [shilingi] tayari, na mkataba ni kwamba ukishalipwa maana yake hilo eneo siyo lako, unapaswa kupisha ili mwekezaji aweze kuliendeleza,” amesema DC Mntenjele.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amesema wameunda kamati maalumu inayopita kujua sababu za baadhi ya watu kuendelea kuwepo kwenye eneo la Komarera wakati wameshapokea malipo ya fidia za mali zao.

Ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa umma kupuuza watu wanaojaribu kuzusha taharuki na kupotosha ukweli wa kinachoendelea katika eneo hilo.

“Watu wanajaribu kutengeneza mazingira ya kuzusha taharuki ionekane kama Serikali imewavunjia wakati wanatakiwa wao wenyewe wavunje waondoke, kwa sababu tayari wamekwishalipwa fidia.

“Kama umeshalipwa maana yake umelipwa kila kitu, kama ni nyumba ilikuwepo umekwishafidiwa, kama ni miti ipo umefidiwa, kwa hiyo vile vitu siyo vyako tena kwa sababu vimeshalipwa, ile ya kukuacha uondoke na mabati yako ni huruma tu.

“Na hili lote linajulikana, hata mheshimiwa mbunge wao anajua na wameshaambiwa kwamba kama ulikwishachukua hela za watu uondoke kwenye eneo husika ili upishe mwekezaji aweze kuendeleza kazi zake,” amesisitiza DC Mntenjele.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Tarime unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages