NEWS

Monday 12 December 2022

TANAPA yang’ara Tuzo ya Ubora wa Kimataifa kwa mara ya 3 mfululizoNa Mwandishi wa TANAPA
-------------------------------------------

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa mara nyingine tena limeshinda Tuzo ya Ubora ya Kimataifa ya Mwaka 2022 – (European Award for Quality Choice Achievement 2022) katika daraja la Diamond inayotolewa na Jumuiya ya Ulaya inayojishughulisha na utafiti wa ubora – European Society for Quality Research (ESQR).

Tuzo hii (pichani juu) ambayo imepokewa usiku wa kuamkia leo na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Massana Mwishawa - Mkuu wa Kanda ya Mashariki na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Beatrice Kessy anayesimamia Maendeleo ya Biashara wakiwa na wenyeji wao Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Juma Salum, Vivian Rutaihwa na Stella Mkude katika hafla ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na ESQR kwenye Hotel ya Le Plaza jijini Brussels, Ubelgiji.

Hii ni ni tuzo ya tatu kutolewa na taasisi hii kwa TANAPA ambapo tuzo ya kwanza ilitolewa mwaka 2020 – “Best Practice Award – GOLD category, mwaka 2021 ilipata tuzo ya “Quality Achievement – PLATINUM category na mwaka huu wa 2022 inapokea tuzo ya Quality Choice – DIAMOND category.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Massana Mwishawa (kushoto) na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Beatrice Kessy wakionesha Tuzo na Cheti cha ushindi huo wa TANAPA.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa ESQR, Michael Harris jumla ya kampuni na taasisi 41 kutoka nchi 31 duniani zimeshirikishwa katika kinyang’anyiro hiki ambapo kwa Tanzania ni TANAPA pekee imeshirikishwa.

“TANAPA imekuwa mshindi wa tuzo ya ubora wa juu katika uhifadhi na huduma za kiutalii,” Harris alitangaza wakati wa kukabidhi tuzo hiyo.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni miongoni mwa hifadhi zilizo chini ya TANAPA

Naye Kaimu Balozi wa Tanzania katika Jumuiya ya Ulaya, Ubeligiji na Luxembourg, Juma Salum aliipongeza TANAPA kwa kazi iliyotukuka ya uhifadhi na huduma za utalii kufikia kiwango cha kutambuliwa na jumuiya za kimataifa.

Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, William Mwakilema alisema inatia moyo kuona jitihada za wahifadhi walioko katika hifadhi za taifa zimetambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

“Bila shaka tuzo hii itachochea mioyo ya wahifadhi wetu kufanya kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu zaidi,” Mwakilema alisema.

Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, William Mwakilema.

Kamishna Mwakilema alisema pia tuzo ya ubora wa juu itawapa imani watalii na wawekezaji juu ya utendaji bora wa nchi yetu katika nyanja ya uhifadhi na utalii.

“Nina imani hii tuzo itakuwa na mchango katika jitihada za Rais wetu Mama Dkt Samia Suluhu Hassan za kuvutia watalii milioni tano kufikia mwaka 2025 kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi,” Mwakilema alisisitiza.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages