
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba.
Tarime
--------------
Kijiji cha Matongo wilayani Tarime kiko mbioni kukamilisha ujenzi wa jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Matongo kwa gharama ya shilingi milioni 172.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Charles Ryoba, fedha hizo zimezotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Mgodi huo unaendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals.
“Fedha hizo zimetolewa na mgodi kupitia CSR, tuko mwishoni kabisa - tumefikia asilimia zaidi ya 90 hivi tuweze kukamilisha ujenzi,” Ryoba ameiambia Mara Online News, leo Mei 3, 2026.
Mwenyekiti huyo amesema mradi huo ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya elimu katika kijiji hicho kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara.
“Tumeshakamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Matongo kwa shilingi milioni 85 na nyumba ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Matongo kwa shilingi milioni 64, fedha zote hizo ni za CSR Barrick North Mara,” amesema.
Aidha, Ryoba amedokeza kuwa kijiji hicho kina mpango wa kuanza uzibuaji wa barabara ya Mashamani yenye urefu wa kilomita zaidi ya mbili, ambao pia utatekelezwa kutokana na fedha za CSR kutoka mgodi huo.
Uzibuaji wa barabara hiyo utasaidia kuhisisha shughuli za kijamii na kiuchumi kijijini Matongo, kwa mujibu wa Mwenyekiti Ryoba.
Kiongozi huyo ameishukuru Barrick North Mara kwa mchango wake katika maendeleo ya kijiji hicho, huku akiendelea kuwahimiza wanakijiji kuendelea kudumisha mahusiano mazuri na mgodi huo.
“Sasa hivi tuna mahusiano yetu kama kijiji na mgodi ni mazuri, ninawaomba wananchi tuendelee kuyadumisha. Mahusiano ndiyo kila kitu,” amesisitiza Ryoba.
Mpaka sasa, mgodi huo umetumia shilingi bilioni 26.86 kugharimia utekelezaji wa miradi ya CSR 255 katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, barabara, maji, miradi ya kiuchumi na mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime - tangu mwaka 2019 ulipokabidhiwa kwa Kampuni ya Barrick.
No comments:
Post a Comment