NEWS

Thursday 29 December 2022

TANAPA yazindua ujenzi wa Uwanja wa Gofu Hifadhi ya Serengeti



Na Mara Online News
------------------------------------

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limezindua na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Uwanja wa Gofu wenye hadhi ya kimataifa katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Hafla ya uzinduzi huo imefanyika leo Desemba 29, 2022 sambamba na uzinduzi wa Kampuni ya Uwekezaji TANAPA (Tanapa Investment Ltd) katika eneo la Fort Ikoma unapojengwa uwanja huo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Jenerali (Mstaafu) George Marwa Waitara amewapongeza na kuwashukuru wajumbe wa bodi hiyo kwa mawazo na michango iliyofanikisha uanzishaji wa miradi hiyo.

Akizungumzia ujenzi wa uwanja huo wa gofu, Jenerari Mstaafu Waitara ambaye ndiye amekuwa mgeni rasmi wa matukio hayo ya kihistoria, amesema umeasisiwa na Bodi ya Wadhamini ya TANAPA kama zao jipya la utalii.

Amebainisha kuwa dhumuni kuu la kuanzisha uwanja huo ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni tano na mapato kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025.

Jenerali Mstaafu Waitara akizungumza katika hafla hiyo

“Kutokana na umaarufu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti tuna kila sababu ya kuamini kwamba zao hili jipya la utalii litakuwa kivutio kikubwa na chachu ya kuongeza mapato yatokanayo na utalii kwenye shirika letu la TANAPA,” amesema Jenerari Mstaafu Waitara.

Ameongeza kuwa uwanja huo unajengwa baada ya upembuzi yakinifu, andiko la biashara na tathmini ya awali ya mazingira kuonesha kwamba hautaathiri mazingira na mwenendo wa wanyamapori katika eneo hilo.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa utalii kutambua uwepo wa uwanja huo, kuutangaza na kupeleka watalii/wacheza gofu.


“Mradi huu unatarajiwa kuvutia wacheza gofu zaidi ya 3,000 kwa mwaka kutoka ndani na nje ya nchi. Aidha, kupitia zao hili, Shirika [TANAPA] linatarajia kupata shilingi bilioni 1.5 mpaka mbili kwa mwaka,” amesema.

Kuhusu Kampuni ya Uwekezaji TANAPA ambayo ndiyo mtekelezaji mkuu wa ujenzi wa uwanja huo, Jenerari Mstaafu Waitara amesema imeanzishwa kwa melekezo ya Serikali ili kutekeleza shughuli mbalimbali za ujenzi ndani na nje ya shirika hilo.


Naye Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, William Mwakilema amesema ujenzi wa Uwanja wa Gofu Hifadhi ya Taifa Serengeti ulianza Oktoba 2022 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2023.

Kwa mujibu wa Kamishna Mwakilema, hadi sasa ujenzi wa uwanja huo umeshagharimu shilingi milioni 520 na unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 7.5 utakapokamilika.

“Utekelezaji wa uwanja huu utafanyika kwa awamu mbili kulingana na upatikanaji wa fedha,” amesema.

Kamishna Mwakilema akizungumza wakti wa hafla hiyo

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Gilman Kasiga ameipongeza TANAPA kwa hatua hiyo akisema itasaidia kuhamasisha na kuendeleza mchezo wa gofu nchini.

Kasiga amesema mchezo wa gofu unafundisha nidhamu na maadili, hivyo unachezwa na mtu yeyote bila kujali uwezo wake wa kiuchumi.

Ameiomba TANAPA kuangalia uwezekano wa kuwashirikisha wanafunzi wa shule zilizo jirani waweze kujifunza mchezo huo.

Aidha, ameahidi kwamba uwanja huo ukikamilika TGU itakuwa inapeleka mashindano ya kitaifa na kimtaifa ya mchezo wa gofu.

Kasiga akizungumza katika hafla hiyo

Viongozi wengine waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa miradi hiyo ya TANAPA ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vincent Mashinji, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Izumbe Msindai, Makamanda wa Uhifadhi wa TANAPA, Martin Loibooki (Kanda ya Magharibi) na Massana Mwishawa (Kanda ya Mashariki).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages