NEWS

Tuesday 6 December 2022

Wenye madai halali waitiwa fidia mgodi wa Barrick North Mara



Na Mara Online News
----------------------------------

MGODI wa Dhahabu wa North Mara umetoa wito wa kuwasihi wananchi wote wenye madai halali kufika katika ofisi zake kuchukua fidia ya mali zao, ili kupisha upanuzi wa shughuli za mgodi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Wito huo ulitolewa jana na Meneja Mahusiano wa Mgodi huo, Gilbert Mworia, wakati Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa alipotembelea eneo linalohitajiwa na mgodi huo katika kijiji cha Nyabichune kilichopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara.

Mworia alisema tayari zimeshatengwa fedha kwa ajili ya kulipa wananchi fidia za mali mbalimbali katika eneo hilo, ambazo zimeshafanyiwa tathmini chini ya usimamizi wa Serikali.

“Tunawashauri waje kuchukua malipo yao, sasa hivi kuna hundi pale ya bilioni 1.8 zinasubiri tangu mwaka huu. Kwa hiyo niwasihi wenye madai ambayo ni genuine (halisi) waje ofisini tuwapatie malipo yao,” alisema Menena Mahusino huyo wa Barrick North Mara.

Alisema Kampuni ya Barrick ina nia njema ya kuwalipa wananchi fidia za mali zao na kuwahamisha kutoka eneo hilo ili kupisha upanuzi wa shughuli za uchimbaji madini.

“Kwa hiyo sisi kama kampuni tuko tayari kukuhamisha kukupeleka sehemu nyingine, lakini hiyo itawezekana kama watu hawatategesha mali mbalimbali kwenye eneo lililokwishafanyiwa uthamini,” Mworia alisisitiza.

Alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba wananchi kuwa tayari kufanyiwa tathmini ya mali zao na kuchukua malipo ya fidia ili kutokwamisha upanuzi wa shughuli za mgodi wa North Mara.

“Mwaka jana kuna watu tulitaka tuwatoe hapa, wako watu wamekataa kufanyiwa uthamini, lakini kuna watu pia tumewafanyia, kuna watu 13 wamegoma hadi hii leo kuchukua malipo yao.

“Sasa watakapokaa kwa miaka kama kumi ijayo hawajachukua malipo, akija sisi tutampa thamani ile ile, wakati huo unakuta miaka mingi imeenda hela haina thamani na huwezi ukaenda kujenga makazi mengine,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Dkt Kiruswa amewataka watu kuacha mara moja kutegesha majengo na mazao mbalimbali kwa nia ya kulipwa fidia katika eneo lililofanyiwa tathmini kijijini Nyabichune ili kupisha shughuli za mgodi huo, la sivyo Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

“Nilishatoa tamko kuhusu madai hewa kwamba yeyote atakapobainika sheria itachukua mkondo wake maana ni sawa na mwizi. Kwa hiyo niendelee kusisitiza kwamba zoezi hili la kuendelea kutegesha haliwezi kuruhusiwa likaendelea bila kuwa na mwisho,” alitahadharisha.

Naibu Waziri Kiruswa akisisitiza tamko kijijini Nyabichune

Wakati huo huo, Naibu Waziri huyo wa Madini amepiga marufuku wananchi kujihusisha na uchimbaji madini katika eneo hilo la Nyabichune lililofanyiwa tathmini, baada ya kubaini kuwa shughuli hizo zinafanyika hadi ndani ya nyumba za makazi ya watu.

“Ninazidi kusisitiza kwamba ni mrufuku kuendelea kuchimba madini katika maeneo haya,” alisema Dkt Kiruswa na kuendelea:

“Ndugu zangu wana-Nybichune, Serikali yenu inawapenda, inataka mtajirike ni sawa kabisa na ni halali mpate maeneo ya kuchimba madini, lakini Serikali yenu haiko tayari kuona mnahatarisha maisha yenu.

“Sisi tuliopewa dhamana na Rais ya kusimamia sekta tutakuwa na melezo ya kutoa kwanini mmewaacha watu wachimbe kwenye makazi yao. Hatuko tayari kuiletea Tanzania aibu hiyo ya kuwacha mchimbe katika mazingira ambayo ni hatarishi kwa maisha yenu kwa kuchimba mashimo ndani ya makazi.”

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages