NEWS

Monday 23 January 2023

Barrick North Mara yaanza kuifanyia German Road maboresho makubwa


Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (katikati) akishuhudia matengenezo yanayoendelea katika Barabara ya German jimboni humo, juzi. (Na Mpigapicha Wetu)

Na Mwandishi Wetu, Tarime
-------------------------------------------

BARABARA ya German (German Road) ambayo imekuwa haipitiki kirahisi kwa miaka mingi katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, hatimaye imeanza kufanyiwa maboresho makubwa kwa gharama za Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupiti Kampuni ya Twiga Minerals.

Uboreshaji wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 45 unatarajiwa kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika jimbo la Tarime Vijijini lenye utajiri mkubwa wa madini.

Utarahisisha huduma za usafiri wa magari ya abiria na mizigo kwa wananchi wanaoishi kata tano [Komswa, Manga, Kiore, Kibasuka na Kemambo] na mgodi wa North Mara kwa upande mwingine.

Kwa mujibu wa Meneja Mradi wa Barrick North Mara, Mhandisi Everest Kivuyo, maboresho ya barabara hiyo yalibuniwa na mgodi huo ili kuwaondolea watumiaji usumbufu wa kupita.

“Mgodi katika mipango yake uliwasiliana na TARURA (Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini) mwaka 2020 wakatusaidia miongozo kwa ajili ya mchoro na mgodi kupitia mchakato wake wa ndani tukapata Mhandisi Mshauri wa mradi huu,” Mhandisi Kivuyo alimweleza Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara alipofanya ziara ya kukagua mendeleo ya ukarabati wa barabara hiyo, juzi.

Alisema barabara hiyo inakarabatiwa kwa kiwango cha changarawe kinachohusisha uwekaji wa makaravati, alama za barabarani na barabara za mchepuko.

Mhandisi Kivuyo alifafanua kuwa utekelezaji wa mradi huo umegawanywa katika vipande vitatu; cha kwanza chenye urefu wa kilomita 15 kikianzia eneo la Gachuma hadi Kembwi, cha pili Nkerege hadi Nyarwana (km 15) na cha tatu Nyarwana hadi Uwanja wa Ndege chenye urefu wa kilomita 15 pia.

“Mradi huu umesanifiwa kwa kiwango cha changarawe lakini pia unahusisha kuinua tuta kwa wastani wa sentimita 30 katika eneo lote na mwisho kabisa litawekwa tabaka ambalo litasaidia magari kupita kwa usalama.

“Lakini pia upana umezingatia maelekezo ya TARURA. Mpaka barabara itakapokuwa inaisha upana wake utakuwa mita nane ukiwa na mifereji ya pembeni na ya kuchepusha maji.

“Pia mradi huu umesanifiwa katika namna ya kuweka makarvati mengi. Kipande cha pili pekee kitkuwa na makaravti 56 yakiwemo 13 mkubwa yenye mtundu mengi.

“Kwa hiyo kutakuwa na mabadiliko makubwa - kwa maana kwamba maji yatakuwaa yakienda bila kupita barabarani kama ilivyokuwa mwanzo,” alisema Mhandisi Kivuyo.

Lucasy Stanley ni Mkurugenzi Stanley Engineering Co. (T) Ltd inayotekeleza mradi huo. Anasema kipande cha Gachuma-Kembwi kilikamilishwa Oktoba 2022.

“Tuna mienzi mitatu tunaendelea na kipande cha pili ambacho tunatarajia kukikamilisha Aprili mwaka huu,” alisema Stanley.

Alisema wanapata ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi na kwamba wameweza kuajiri watu 150 wakiwemo zaidi ya 100 ambao ni wenyeji wa maeneo hayo.

Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Ngusa Shira alisema utekelezaji wa mradi huo unaendele vizuri.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara aliipongeza na kuishukuru Barrick North Mara kwa kuona umuhimu wa kuifanyia German Road maboresho makubwa.

“Hii barabara ilikuwa na malalamiko mengi kwa maana kwamba ilikuwa imekaa muda mrefu haijakarabatiwa. Kwa hiyo kwa niaba ya wananchi ninaushukuru mgodi kwa kuchukua hatua ya kuboresha barabara hii.

“Kupata msaada wa kujengewa barabara ya kilomita 45 sio jambo dogo. Kwa hiyo mimi hili ni jambo muhimu sana la kujenga barabara hii ambayo ilikuwa na malalamiko,” alisema Waitara.

Pia Mbunge Waitara aliupongeza mgodi na mkandarasi kwa kuwapa wananchi wenyeji wa maeneo ya mradi huo kipaumbelea katika suala zima la ajira.

“Nilikuwa nauliza vijana wetu hapa kujua wananufaika namna gani na mradi huu, hasa wale wenye uwezo wa kufanya kazi, nimefurahi kusikia taarifa hapa kwamba wamepata ajira na hawana changamoto ya mahusino.

“Nimeambiwa pia kwamba hakuna udokozi, maana watu wengine wakifanya kazi mahali kunakuwa na hoja za malalamiko ya udokozi ambayo yanasababisha vijana wenyeji wasipate kazi.

“Kwa hiyo nilihoji vijana hapa wakaniambia wamepata kazi na hawajapata usumbufu wa mlipo na hilo limeendelea kutengeneza mhusiano mzuri katika eneo hili,” alisema Waitara.

Matumaini yake ni kwamba mgodi huo utakuwa na utaratibu wa kukarabati barabara hiyo mara kwa mara ili isiharibike tena kama mwanzo.

Hata hivyo pamoja na hatua hiyo, mbunge huyo aliuomba uongozi wa Barrick North Mara kufikiria uwezekano wa kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kuondokana na ukarabati wa mara kwa mara.

“Hii barabara ni kweli kwa sasa inatengenezwa kwa kiwango cha changarwe kama ilivyoelezwa na tunatarajia kwamba itaenda kwa mkataba kama mlivyokubaliana na baadaye mnaweza kuitumia kwa manufaa mkubwa.

“Kwa hiyo tunaomba hii barabara muiweke kwenye mipango yenu hata kama itakuwa ni kwa vipande vipande, hii barabara inapaswa kujengwa kwa kiwango cha lami. Mtatumia pesa kubwa sana - kila mwaka mnamwaga changarawe, mnaweka mawe, mnaweka makaravati, lakini mkijenga kwa lami itatumu muda mrefu ikiwa imara,” alisema Mbunge Waitara.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages