NEWS

Tuesday 10 January 2023

Chandi ampa tano Rais Samia kuruhusu mikutano ya hadhara, azungumzia faida za Royal Tour



Na Mwandishi Wetu, Serengeti
--------------------------------------------

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa (pichani juu katikati), amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu mikutano ya kisiasa ya hadhara nchini, akisema chama hicho tawala kimejipanga kusimamia kikamilifu utekelezaji wa ilani yake.

“Tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt Samia kwa kushiriki demokrasia ya ushindani wa vyama vingi, tumejipanga vizuri kusimamia ilani ya CCM kwa asilimia 100 na kwa sasa utekelezaji wake kwa mkoa wa Mara uko asilimia 75,” amesema Chandi wakati kihitimisha hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano la Royal Tour na Fursa za Kiuchumi Mara lililofanyika mjini Mugumu, Serengeti leo.

Aidha, Chandi ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuwataka wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kuyasemea kwa ufasaha maendeleo ya kisekta yanayowezeshwa na Serikali pamoja na chama hicho.


Akizungumzia kongamano hilo lililoandaliwa na Taasisi ya Global Peace Advocate for Conflicts Resolution, Mwenyekiti huyo wa CCM Mara amesema Rais Samia anastahili pongezi kubwa kwa kutengeneza Filamu ya The Royal Tour na uzalendo wa kuongoza nchi kwa namna ya kipekee inayoimarisha mshikamano wa Watanzania kwa amani.

“Kwa kweli kuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia kwa matokeo chanya ya Filamu ya The Royal Tour, ziko fursa nyingi zilizoongezeka nchini baada ya filamu hii.

“Kwa kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM inatuelekeza tutengeneze ajira milioni nane, kwa nafasi yangu ya Uenyekiti wa CCM Mkoa nitasimamia na kuhakikisha fursa za ajira zitokanazo na filamu hii zinapatikana na kuwanufaisha wana-Mara kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais,” amesema Chandi.


Kutokana na asilimia 77 ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwa ndani ya mkoa wa Mara, Mwenyekiti Chandi ameziomba mamlaka za TANAPA, TAWA na wadau wanaohusika na uifadhi kuwapa kipaumbele wakazi wa vijiji vilivyo jirani na hifadhi hiyo katika ajira na fursa mbalimbali.

“Mfano kuuna fursa za kuuza matunda, mbogamboga na bidhaa nyingine muhimu katika hoteli zilizo ndani ya hifadhi hii, naomba watu wetu wanufaike kwa kuuza bidhaa hizo huko kwa kuwa katika mkoa wetu wa Mara zinapatikana kwa wingi na ni bora,” amesema Chandi.

Amewahimiza vijana wa mkoani Mara kuchangamkia fursa zilizopo na kutokata tamaa. “Kwa kuwa nimepokea leo andiko la ujenzi wa uwanja wa mpira najua kwa njia hiyo pia tutavutia utalii wa ndani, hivyo akina mama na wasafirishaji pia mchangamkie fursa,” amesema na kuendelea:

“Andiko hili ni sehemu ya kutekeleza agizo la Mwenyekiti wetu wa Taifa kuhusu Chama [CCM] kuwa na miradi ya kiuchumi ili kuondokana na utegemezi.”


Kwa upande wa upande wa elimu, Chandi amesema Rais Samia ameshatekeleza ahadi ya kujenga vyumba vya madarasa vya kutosha na wanafunzi wote wanaofaulu kuingia kidato cha kwanza wanapata nafasi kusoma.

“Aidha, wanaofaulu kuingia vyuo vikuu Mheshimiwa Rais Samia ameweka mazingira safi ya kupata mikopo ya elimu ya juu.

“Kwenye Afya Mheshimiwa Rais amejenga vituo vya afya vya kutosha na bado vinaendelea kujengwa pale ambapo hakuna, lengo ni kila kata iwe na kituo cha afya na kuimarisha huduma za afya katika Jamii.

“Kwenye miundombinu ya barabara, tayari barabara ya Nata-Mugumu yenye urefu wa kilomita 35 kwa kiwango cha lami mkataba umeshasainiwa na wakati wowote mkandarasi ataanza kazi, barabara ya lami Tarime-Serengeti tayari mkandarasi yuko kazini.

“Kwa vile ilani ya CCM inaelekeza kujenga miundombinu ya usafirishaji na kuunganisha mikoa, CCM Mkoa wa Mara tuna mpango wa kumuomba Mheshimiwa Rais Samia na sisi atujengee reli ya kisasa kutoka Simiyu kuja Mara.

“Kwa upande wa wakulima na wafugaji, mahindi ya bei nafuu yameletwa mkoani kwetu ili kunusuru kaya ambazo zimeathirika na njaa na hata hapa Serengeti mahindi hayo yapo, na mikopo yenye riba nafuu kwa wafugaji imeendelea kutolewa hata hapa Serengeti.

“Kuhusu mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu - mikopo ya asilimia 10 imeendelea kutolewa na walengwa wa TASAF (kaya maskini) wanaendelea kunufaika ili kujikomboa kutoka kwenye mazingira magumu,” amesema Mwenyekiti Chandi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages