
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho.
Mara Online News
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amewaomba wananchi watakaolipwa fidia kupisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti kuhakikisha wanahama kwa wakati ili mkandarasi aanze kutekeleza mradi huo wa kimkakati.
Amewaomba kutoa ushirikiano pia kwenye uthaminishaji wa mali zao, ikiwa ni pamoja na kuepuka vishawishi vya kupandisha bei, hali inayoweza kusababisha mgogoro na ucheleweshaji wa mradi huo.
Akizungumza na wakazi wa mji wa Mugumu, wilayani Serengeti jana, Dkt. Nyansaho alisema wataalamu wamekuja kuangalia upya uthaminishaji ili serikali iwalipe fidia stahiki.
“Haki itatendeka kwenye tathmini, lakini na ninyi jamani msije mkafanya kama biashara, ukishalipwa ondoka, kwa sababu mkandarasi hawezi kuja site (eneo la mradi) kabla hamjaondoka,” alisema.
Waziri Nyansaho ambaye ni mwenyeji wa Serengeti, alisema uwanja huo utarahisisha usafiri wa anga na kuongeza mzunguko wa shughuli za kiuchumi, hususan kwa sekta ya utalii inayotegemea uhifadhi wa wanyamapori.
Kwa mujibu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mpango wa ujenzi wa uwanja huo umepewa kipaumbele kwa kuingizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya chama tawala - CCM ya mwaka 2025-2030.
Tayari Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imeshatiliana saini na Kampuni ya Saba Engineering mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo katika mji wa Mugumu.
Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Abdul Mambokaleo, serikali ilitenga shilingi bilioni 1.3 katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uwanja huo.
Inaelezwa kuwa ujenzi wa uwanja huo umebuniwa kuwa wa kisasa, ukiwa na hudumu zote muhimu zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Serikali inadhamiria kujenga mradi huo ili kukuza sekta ya utalii kwa kuongeza idadi ya watalii kutoka mataifa mbalimbali wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Ujenzi wa uwanja huo utawezesha watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani kutua moja kwa moja katika mji wa Mugumu na hivyo kuufanya kuwa kitovu cha utalii.
Lakini pia, uwanja huo utavutia uwekezaji zaidi katika wilaya hiyo ambayo imejaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na mapori ya akiba ya Ikorongo- Grumeti.
Vilevile, mradi huo unatarajiwa kutengeneza fursa za kiuchumi, zikiwemo ajira kwa vijana, huduma za malazi, chakula na usafirishaji - zitakazokuwa na mchango mkubwa katika kuinua kipato cha wananchi.
Kwa ujumla, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Serengeti unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi, kwa kuchochea biashara, utalii, ajira na fursa za uwekezaji kwa wakazi wa mji wa Mugumu na wilaya ya Serengeti.
No comments:
Post a Comment