NEWS

Friday 6 January 2023

Kamati ya Usuluhishi yaongeza idadi ya waliochukua fidia Komarera kupisha mgodi wa Barrick North Mara, watu 4,881 walipwa bilioni 21.594/-


Na Mwandishi Wetu, Tarime
--------------------------------------------

IDADI ya watu waliolipwa fidia za mali zao katika eneo la Komarera ili kupisha upanuzi wa shughuli za Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, imeongezeka kutoka 4,836 hadi 4,881, baada ya Kamati ya Usuluhishi kuelimisha wananchi 45 waliokuwa wamegoma wakakubali kwenda kupokea malipo yao.

Mpaka sasa Kampuni ya Barrick inayoendesha mgodi huo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals, imekwishatumia shilingi bilioni 21.594 kulipa wananchi hao 4,881.

Kwa mujibu wa Mthamini wa Serikali, Rashid Magetta, wananchi hao 4,881 ni miongoni mwa 5,162 walio kwenye orodha ya kulipwa fidia za mali zao mbalimbali zilizokutwa kwenye eneo la Komarera.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ntarechagini katika kijiji cha Komarera, Marwa Mwita Omuko amewambia waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo leo Januari 6, 2023 kwamba baadhi wakazi wa kitongoji hicho ni miongoni mwa watu walioelimishwa na Kamati ya Usuluhishi wakakubali kwenda kuchukua malipo ya fidia za mali zao.

Marwa Mwita Omuko akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la Komarera

“Kwa mfano bibi yangu baada ya hii Kamati kumuelimisha anachostahili kulipwa na asichostahili kulipwa ameenda amechukua, lakini wengie hawajaenda kuchukua kwa madai kuwa kiwango cha fidia zao ni kidogo kuliko walivyotarajia,” amesema Omuko.

Waandishi wa habari wameshuhudia mitambo ya Barrich North Mara ikiendelea kusafisha eneo la Komarera, ikiwa ni pamoja na kuondoa majengo ya watu waliohama baada ya kupokea malipo ya fidia.


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Usuluhishi iliyoundwa na Serikali, amesema wanaendelea kuhamasisha wananchi waliochukua malipo ya fidia za mali zao kuondoka kwa hiari, ili kutokwamisha mgodi wa Barrick North Mara kupanua shughuli zake za uchimbani madini.

“Tunawasihi wale ambao tayari wameshachukua hela waendelee kuondoka ili mgodi uendelee kufanya usafi katika eneo hili na hatimye uweze kuendelea kuwekeza. Hatubomoi kwa mtu ambaye bado yuko ndani lakini kwa yule ambaye ameshaondoka tunabomoa boma lake,” Kanali Mntenjele katika mazungumzo na waandishi wa habari.

Mkuu huyo wa wilaya ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuwatahadharisha wananchi kuwa makini na watu wanaojaribu kuingiza siasa na kupotosha ukweli wa kinachoendelea katika eneo la Komrera.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele.

“Kuna wanasiasa wanaingiza siasa humu - jambo ambalo siyo jema kwa sababu hapa ni uhalisia, mtu analipa kulingana na kitu kilichokuwepo awali.

“Sasa kama umeendelea kuendeleza wakati katazo lilishafanyika siyo halali. Ukianza kuingiza siasa na mkiwasikiliza wanasiasa mtapoteza muda wenu badala ya kuondoka mwende mkafanye maendeleo kwingine ili mgodi nao uendelee kufanya shughuli zake.

“Na tuelewe pia kwamba mgodi huu [North Mara] una ubia na Serikali kupitia Twiga Minerals. Sasa kuendelea kuwepo [katika eneo la Komarera] maana yake mnaikwamisha Serikali na mnakwamisha mwekezaji asiendelee kufanya kazi zake,” amesisitiza Kanali Mntenjele.

Kwa mujibu wa Mthamini wa Serikali, Magetta, kuna watu wachache ambao baada ya kulipwa fidia za nyumba zao walikosa uaminifu wakazipangisha kwa wengine kabla ya usafishaji kuanza katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages