NEWS

Tuesday 31 January 2023

Mbunge Waitara atumia maadhimisho ya miaka 46 ya CCM kumjibu Heche, aweka hadharani maendeleo ya kisekta aliyowezesha Tarime Vijijini


Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara.

Na Mwandishi Wetu, Tarime
-------------------------------------------

MBUNGE wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ametumia mkutano wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM, kujibu kauli dhidi yake zilizotolewa hivi karibuni na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA, John Heche.

Huku akijiita mwanasiasa na kiongozi wa viwango vya juu, Mbunge Waitara ametumia muda mwingi jukwaani kutaja miradi chungu nzima iliyotekelezwa katika kipindi cha uongozi wake wa miaka miwili Tarime Vijijini, ambayo haikuwepo enzi za uongozi wa Heche aliyeongoza jimbo hilo kwa miaka mitano mfululizo (2015 hadi 2020).

“Katika kipindi changu tumepata shilingi zaidi ya bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ICU ya Nyamwaga imejengwa, tumepata ujenzi wa barabara ya lami kilomita 25 kutoka Mogabiri hadi Kwinogo - mkandarasi yuko site (eneo la mradi),” Waitara amesema katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kimkoa kwenye uwanja wa “Shamba la Bibi” mjini Tarime leo.

Ametaja miradi mingine iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa karibu kila kijiji na kata kuwa ni ya elimu, afya, maji, umeme na barabara za lami na changarawe.

Baadhi ya mirdi hiyo, kwa mujibu wa Waitara, inatekelezwa kutokana na mabiliyoni ya fedha za Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na Kapuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

“Mama Samia [Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan] ametutendea wema sana watu wa Tarime Vijijini,” amesema Mbunge Waitara.

Jambo jingine ambalo Mbunge Waitara anajivunia ni ushawishi wake uliowezesha mabilioni ya fedha za CSR Barrick North Mara kusambazwa katika vijiji na kata zote za jimbo la Tarime Vijijini, tofauti na miaka ya nyuma kabla ya uongozi wake, ambapo zilikuwa zinaelekezwa kwenye kata tano zenye vijiji 11 pekee vilivyo jirani na mgadi huo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi (wa pili kushoto) na viongozi wengine wakifuatilia jambo mkutanoni leo

“Tumeubana mgodi unajenga barabara ya German yenye urefu wa kilomita 45 kwa kiwango cha changarawe, na mwakani utaanza kuijenga kwa kiwango cha lami.

“Mimi viwango vyangu ni vya kimataifa, nafanya siasa ya nidhamu, nafanya siasa ya maendeleo, siwezi kuwachonganisha wananchi na serikali, kama ni jiwe nitasema ni jiwe kama ni kisu nitasema ni kisu, nataka nifundishe watu adabu ya siasa,” ametamba Mbunge Waitara.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi, amewataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia katika juhudi za kuwaletea maendeleo ya kisekta.

Hivi karibuni, akizungumza akwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe uliofanyika kwenye uwanja huo wa “Shamba la Bibi”, Heche ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini, alitoa maneno yaliyotafsiriwa kuwa ni matusi na udhalilishaji dhidi ya Mbunge Waitara.

Katika sehemu ya mazungumzo yake, Heche alitumia lugha ya asili kutoa maneno yaliyotafsiriwa kuwa ni matusi yanayomlenga moja kwa moja Mbunge Waitara, ingawa hakumtaja jina.

Maneno hayo ambayo Heche alitamka kwa lugha ya Kikurya hatuwezi kuyachapisha kwa sababu za kimaadili.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages