NEWS

Tuesday 31 January 2023

Chandi agusia mgogoro wa wanavijiji Tarime na Hifadhi ya Serengeti akihutubia madhimisho ya miaka 46 ya CCM yaliyoandaliwa na UWT MaraNa Mwandisi Wetu, Serengeti
--------------------------------------------

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi (wa pili kulia pichni juu), amesema amezungumza na mawaziri wenye dhamana ya ardhi na maliasili na utalii kuwaomba washughulikie haraka utatuzi wa mgogoro uliopo kati ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na baadhi ya vijiji vinavyopakana nayo katika wilaya ya Tarime.

Chandi aliyasema hayo wakati akihutubia wananchi katika maadhimisho ya Miaka 46 ya Kumbukumbu ya Kuzaliwa kwa CCM - yaliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) CCM Mkoa wa Mara na kufanyika kwenye viwanja vya stendi ya Mugumu wilayani Serengeti jana.

“Nimeongea juzi na Waziri wa Maliasili na Utalii, na Waziri wa Ardhi ili kutatua mgogoro uliopo kati ya Hifadhi ya Serengeti na wananchi wa Tarime na Serengeti,” alisema mwenyekiti huyo.Aidha, Chandi alitumia nafasi hiyo pia kuelezea maendeleo makubwa ya kisekta yaliyowezeshwa mkoani Mara chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.

Aliyataja maendeleo hayo kuwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa vya kutosha katika shule za msingi na sekondari, vituo vya afya, hospitali, barabara za lami na mradi wa umwagiliaji Mugango.

“Niwaombe wananchi wangu wa mkoa wa Mara, malipo pekee ya kumlipa Rais Samia ni kumjazia kura za kutosha mwaka 2025, tukianza na uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024,” alisema Chandi.

Lakini kwa upande mwingine, Chandi aliielekeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kushughulikia haraka uboreshaji wa barabara za mitaa na vijiji zilizoharibika na kusababisha usumbufu kwa wananchi.

Kuhusu ruhusa ya mikutano ya hadhara ya kisiasa iliyotolewa na Rais Samia hivi karibuni, Bosi huyo wa CCM Mara alisema wamejipanga vizuri kukabiliana na hoja za wapinzani majukwaani kwa kauli za kistaarabu.

Awali, Mwenyekiti huyo na viongozi wa UWT Mkoa wa Mara na Wilaya ya Serengeti walitembelea kituo cha Nyumba Salama Mugumu kinachoendeshwa na Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, ambapo viongozi wa Umoja huo walikabidhi msaada wa taulo za kike na sabuni kwa ajili ya wasichana wanaohudumiwa kituoni hapo.

Chandi alimpongeza Mkurugenzi wa Shirika hilo, Rhobi Samwelly ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa kwa juhudi kubwa anazofanya katika kupambana na vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia miongoni mwa jamii.

Pia Chandi alikwenda kuzindua Tawi la CCM Kijiwe cha Wanamama Mugumu Kati na kuongozana na viongozi hao wa UWT kutembelea wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Serengeti na kupanda miti.

Akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Serengeti, Mwenyekiti Chandi aliagiza ijengewe uzio kwa ajili ya usalama, huduma za mtibabu ziimarishwe na eneo hilo liwe na hati miliki.

Alimpongeza Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt Emiliana Donald kwa kazi nzuri anayoifanya.

Leo Januari 31, 2023 Mwenyekiti Chandi ni mgeni rasmi wa Maandismisho ya Miaka 46 ya Kumbukumbu ya Kuzaliwa kwa CCM yanayofanyika kimkoa kwenye viwanja vya “Shamba la Bibi” mjini Tarime.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages