NEWS

Monday 30 January 2023

Mbunge Waitara kumjibu Heche kesho


Mbunge Mwita Waitara

Na Mwandishi Wetu
---------------------------------

MBUNGE wa Jimbo la Tarime Vijijni, Mwita Waitara (CCM), amesema kesho [Jumanne] ataeleza mafanikio yake kwa kipindi cha miaka miwili didhi ya miaka mitano ya mtangulizi wake, John Heche (CHADEMA) aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo mwaka 2015 hadi 2020.

Kwamba ataanika mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake kwenye jimbo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini, miongoni mwa maliasili nyingine.

“Jumanne tarehe 31, mwaka huu tutakuwa na sherehe za maadhimisho ya Miaka 46 ya CCM ambazo zitafanyika Tarime, na moja ya jambo nitakalofanya ni kueleza mafanikio yangu ya ubunge kwa kipindi cha miaka miwili jimboni,” Waitara aliimbia Sauti ya Mara kwa njia ya simu, jana.

Sherehe hizo alisema zinatafanyika mjini Tarime, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa.

Waitara alisema atatumia mkutano huo kumjibu Heche kisomi.

“Kumjibu Heche kisomi ni kwamba nitafanya tathmini ya kazi za Heche kwa miaka mitano jimbo la Tarime Vijijini na kazi za Waitara miaka miwili jimbo la Tarime Vijijini,” alisema mbunge huyo ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri katika wizara mbalimbali miaka ya hivi karibuni.

Alitoa wito kwa wananchi wa Tarime kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo ambao utafanyika kwenye uwanja wa “Shamba la Bibi” mijini Tarime, kwa mujibu wa Katibu wa Uenezi wa CCM Wilaya ya Tarime, Marema Sollo.

Wiki iliyopita, Waitara alikaririwa kwenye vyombo vya habari likiwemo gazeti hili akisema atajibu kauli za Heche ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA - alizozitoa didhi yake katika mkutano wa hadhara wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, uliofanyika kwenye uwanja huo Januari 23, 2023.

Baadhi ya kauli alizotoa kwa lugha ya Kikurya ambazo gazeti hili haliwezi kuzichapa kwa sababu za kimaadili, zilitafsiriwa kuwa ni matusi dhidi ya Waitara.

“Nimepokea simu za watu mbalimbali, watu wame- mind (hawajafurahi), lakini nikasema kwa kuwa ameshazungumza ya kwake, mimi nitapata fursa ya kumjibu publically (hadharani) na mimi nitamjibu kisomi, wala siwezi kumjibu kwa kumtukana - nitamjibu kisomi,” alisema Waitara siku moja baada ya mkutano huo.

Hata hivyo Baada ya Heche na viongozi wengine kuzungumza, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe alihutubia mkutano huo, ambapo aliendelea kusisitiza kauli yake ya kuwataka wanachama wa chama hicho kuepuka chuki za kisiasa dhidi ya Watanzania wenzao.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages