NEWS

Sunday 29 January 2023

Ushirika wa WAMACU wapokea wanachama wapya, wapania mageuzi makubwa ya kiuchumi kupitia kilimo cha mazao ya kimkakati



Na Mwandishi Wetu
---------------------------------

CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Mara (WAMACU LTD) kimepokea wanachama wake wapya 19 ambao ni Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS).

AMCOS hizo ambazo zimejiunga na WAMACU LTD ni Nyakoi kutoka wilaya ya Rorya, Chapa Kazi, Nyansurura, Inuka, Ngarawani, Musati, Mbalibali, Nyamitita, Nyamakendo, Mshikamano, Nguvu Moja, Kisangura, Machochwe, Nyambisa, Jembe ni Mali, Kwanina, Ikorongo, Kenyamonta na Kenyana B zinazojishughulisha na kilimo cha tumbaku wilayani Serengeti.

Wanachama hao walipokewa kupitia Mkutano Mkuu wa 13 wa Mwaka wa WAMACU LTD uliofanyika mjini Tarime, wiki iliyopita.

Kwa mapokezi hayo ya wanachama wapya 19, Ushirika huo wa WAMACU sasa unakuwa na jumla ya wanachama 46 kutoka wilaya mbalimbali za mkoa wa Mara.

AMCOS 27 zilizokuwa wanachama wa WAMACU LTD kabla ya hizo mpya ni Gorong’a, Kema, Itiryo, Kangariani, Bungurere, Muriba, Nyantira, Tagare, Mori, Kemakorere, Nyamwigoma, Mogabiri na Nkongore.

Nyingine ni Nyandurumo, Mwesu, Sirari, Nyakonga, Mbogi, Shadabi, Maisome, Mwibagi, Kitembe, Uwaabu, Mirare, Rabuor, Ring’wani na Nyamatoke ambazo zinajishughulisha zaidi na kilimo cha kahawa.

Hata hivyo akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya WAMACU LTD, David Hechei alisema Ushirika huo una mpango wa kuongeza wanachama zaidi na kupanua wigo wa kuzalisha mazao mengine ya kimkakati ikiwemo alizeti, pamba na pilipili ili kuongeza tija kwa wakulima.

Mgeni rasmi wa Mkutano Mkuu huo wa WAMACU LTD alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vincent Mashinji aliyeambatana na mwenyeji wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, miongoni mwa viongozi wengine.

Katika hotuba yake, Dkt Mashinji alikazia rai iliyotolewa na Kanali Mntenjele ya kuhamasisha vijana kujiunga na vyama vya ushirika ikiwemo WAMACU LTD kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.

“Turidhishe watoto wetu kwenye ushirika kwani dunia ya sasa ni ya ushirika. Mataifa makubwa na yenye nguvu ya kifedha duniani yanaunda ushirika, na ushirika kwa dunia ya sasa ni suala linalohusu usalama wa taifa.

“Kuna siku itafika huwezi kuuza mchicha sokoni kama hutokani na ushirika, hakuna biashara yoyote itakayofanyika nje ya ushirika,” Dkt Mashinji alisisitiza.

Aliwataka maofisa ugani kuhamasisha uanzishaji na uendelezaji wa mashamba darasa ya kilimo na ufugaji ili kushawishi vijana wengi kujiunga na shughuli hizo vijijini.

Dkt Mashinji akizungumza katika mkutno huo

Dkt Mashinji alisema suala la kuimarisha ushirika ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Msimamizi Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni, Kassim Majaliwa.

Hivyo aliwataka wanachama wa WAMACU LTD kuhakikisha kuwa wanauza mazao yao ya kilimo kwenye Ushirika huo na kuepuka kuyauza nje ya nchi bila kuwa na vibali vinavyotolewa na mamlaka za serikali.

Sambamba na hilo Dkt Mashinji aliwakumbusha wakulima kuzingatia pia maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji. “Msilime kwenye vyanzo vya maji,” alionya.

Kuhusu wanaolima tumbaku alisema lazima wawe na mipango endelevu ya kupanda miti kwa ajili ya kuni za kukaushia zao hilo la biashara.

Katika hatua nyingine, Dkt Mashinji aliwahimiza wanachama wa WAMACU LTD kuchangamkia ununuzi wa mbolea ya ruzuku inayotolewa na serikali kupitia Ushirika huo.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya ushirika Tanzania (TFC), Alex Ndikile aliwahamasisha wanachama wa Ushirika huo kujenga utamaduni wa kushiriki maonesho ya Nanenane kila mwaka kwa ajili ya kutangaza shughuli zao na kujifunza kutoka kwa wengine mbinu za uzalishaji wenye tija.

Ndikile alisema sekta ya kilimo haina budi kuendelezwa kwa teknolojia ya kisasa kwani ina mchango mkubwa katika kuzalisha ajira kwa wananchi, kuchangia pato la taifa, usalama wa chakula na uhakika wa malighafi za viwanda.

Katibu huyo alitumia nafasi hiyo pia kuitangaza WAMACU LTD kuwa Wakala wa Bima za Shirikisho hilo mkoani Mara.

Ndikile akizungumz mkutanoni

Mtaalamu Mshauri kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Stanley Rubalila yeye aliishauri WAMACU LTD kufikiria uwezekano wa kuanzisha mradi wa mitambo ya kukaanga kahawa kwa ajili ya matumizi ya watu.

Wajumbe wa mkutano huo ulioongozwa na Mwita Ndege kutoka AMCOS ya Tagare, walithibitisha Muhtasari wa Mkutano Mkuu wa 12 wa Mwaka wa WAMACU LTD uliosomwa na Meneja Mkuu (GM) wa Ushirika huo, Samwel Gisiboye.

Pia walipokea, wakajadili na kuidhinisha yatokanayo na kumbukumbu za mkutano huo wa 12, ikiwemo maazimio mbalimbali na utekelezaji wake.

GM Gisiboye pia aliwasilisha ajenda ya kupokea, kujadili na kuidhinisha taarifa ya utekelezaji ya Bodi ya WAMACU LTD kwa kipindi cha msimu wa mwaka 2022/2023.

Taarifa hiyo ilihusisha makisio ya Ushirika huo kwa mwaka 2023/2024 yaliyoainishwa kwenye mpango mkakati ambao pia ulipitishwa na wajumbe wa mkutano huo wa wiki iliyopita.

Malengo ya mpango mpango mkakati huo wa WAMACU LTD yalitajwa kuwa ni pamoja na kuhamasisha upandaji wa kahawa na mazao mengine ya kimkakati ili kuongeza uzalishaji na mapato yenye tija kwa kila mkulima.

Pia kutoa kutoa elimu ya ushirika na kuongeza wanachma wanaozalisha mazao ya kimkakati yanayostawi katika ukanda wa Mara kama vile kahawa, tumbaku, alizeti na pilipili, miongoni mwa mengine.

“Kuwapa wanachama elimu ihusuyo bidhaa zinazoongeza tija katika kilimo, hasa pembejeo kama mbolea, viuatilifu, mbegu, afya ya udongo, n.k. Kuimarisha uwezo wa kutafuta na kusimamia rasilimali fedha na kuendeleza mahusiano mazuri na wadau wetu wote,” iliongeza taarifa hiyo.

Ajenda nyingine iliyopokewa, ikajadiliwa na kuidhinishwa katika mkutano huo ni ya ukaguzi wa hesabu za WAMACU LTD za mwaka 2022/2023.

Awali, hoja za ukaguzi zilionesha kwamba Ushirika huo umepata hati yenye mashaka, lakini baadaye ilielezwa kuwa dosari zilizokuwepo zimesharekebishwa, hivyo kinachokwenda kutolewa na hati safi.

Wajumbe pia walijadili na kupitisha taarifa ya makisio ya mapato na mtumizi (bajeti) ya Ushirika wa WAMACU LTD kwa msimu wa mwaka 2023/2024 kwa ajili ya utekelezaji wa mipango kazi yake.

Kulingana na taarifa hiyo, mapato ya mauzo ya kahawa safi kwa msimu huo yanakadiriwa kuwa shilingi bilioni 6.622. Kahawa hiyo ni itakayochakatwa ndani ya Ushirika huo baada ya kukusanywa kutoka kwenye Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMGOS).

Makisio ya matumizi kwa ajili ya shughuli za kibiashara, hasa ukusanyaji na uuzaji wa kahawa yanakadiriwa kuwa shilingi bilioni 5.729, kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na GM Gisiboye.

Baadaye Mrajis Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Mara, Emmanuel Rutatora alihitimisha Mkutano Mkuu huo wa 13 wa Mwaka wa WAMACU LTD kwa kukitaka chama hicho kusimamia vizuri utekelezaji wa malengo yake na wakulima kwa ujumla ili kuongeza tija katika sekya hiyo mkoani Mara.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages