NEWS

Wednesday 25 January 2023

Prof Muhongo aongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa sekondari kijijini Muhoji


Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo (mwenye shati jeupe katikati waliosimama) akihamasisha wananchi kuchangia ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika kijiji cha Muhoji jimboni humo, jana. (Na Mpigapicha Wetu)

Na Mwandishi Wetu, Musoma
-------------------------------------------

MBUNGE wa Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa shule ya sekondari mpya katika kijiji cha Muhoji katani Bugwema.

Harambee hiyo ilifanyika jana, ambapo Prof Muhongo alichangia saruji mifuko 150, huku Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt Halfan Haule akichangia saruji mifuko 20 na kushiriki shughuli za ufyatuaji wa matofali.

Kwa upande wao, wanakijijiji wakiongozwa na Diwani wa Kata ya Bugwema, Clifford Machumu waliweza kuchangia saruji mifuko 124 na fedha taslimu kiasi cha shilingi 305,000.

“Michango hiyo ya wanakijiji ni mbali na nguvukazi yao ya kusomba mawe, mchanga na kokoto, pamoja na shilingi 45,000 kutoka kwa kila kaya,” ilieleza sehemu ya taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, leo.

Mbunge Muhongo ambaye aliahidi kuendelea kuchangia ujenzi wa shule hiyo aliwashukuru wote waliochangia vifaa na fedha taslimu katika harambee hiyo.

Kijiji cha Muhoji ni miongoni mwa vijiji vinne vinavyounda kata ya Bugwema, vingine vikiwa ni Masinono, Kinyang'erere na Bugwema.

Kata hiyo ina sekondari moja iitwayo Bugwema ambayo kwa sasa imeelemewa; ambapo wanafunzi wa kidato cha kwanza waliopokewa mwaka huu wa 2023 ni 362 waliogawanywa kwenye mikondo saba, huku jumla ya wanafunzi wote wkiwa 748 na walimu 10.

“Mbali ya mirundikano hiyo kwenye Bugwema Sekondari, bado wanafunzi kutoka kijiji cha Muhoji wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 24 hadi 30 kwenda na kurudu kutoka masomoni,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Malengo ya harambee hiyo ni kuwezesha ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, ofisi mbili za walimu na choo chenye matundu manane - na ukamilike kabla ya Julai 30, 2023 ili Shule ya Sekondari Muhoji ifunguliwe Januari 2024.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages