NEWS

Wednesday, 4 February 2026

Tarime Mji: Ajali ya barabarani yakatisha maisha ya Diwani wa Ketare



Diwani wa Kata ya Ketare, Philipo Marwa Gikaro, akiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani mjini Tarime jana Jumanne.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
---------------

Diwani wa Kata ya Ketare katika Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara, Philipo Marwa Gikaro (CCM), amefariki dunia baada ya kupata ajali ya kugongwa na gari.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Thobias Elias Ghati, amewambia waandishi wa habari leo Jumatano kwamba Philipo amefikwa na mauti wakati akipatiwa matibabu katika Hospital ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kwangwa, mjini Musoma - Mara.

Inaelezwa diwani huyu aligongwa na gari jana Jumanne jioni eneo la Kibumaye wakati akielekea nyumbani kwake Moghabiri, muda mfupi baada ya kuhudhuria kikao cha Baraza la Madiwani kilichopitisha rasmu ya bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka 2026/2027.

Mwenyekiti Thobias amesema tayari mwili wa Philipo umesafirishwa kutoka Musoma na kuhifadhiwa chumba cha maiti katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime (Bomani).

"Mimi na baadhi ya madiwani tupo na familia yake tukiandaa taratibu za mazishi," amesema Thobias.

Mara Online News inaendelea na juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime-Rorya kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo kwa kina.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages