NEWS

Friday 10 February 2023

Kikao cha SHIMMUTA Taifa chafanyika Barrick North Mara


Mwenyekiti wa SHIMMUTA Taifa, Roselyne Massam akizungumza kikaoni.

Na Mwandishi Wetu, Mara
---------------------------------------

KAMPUNI ya Barrick North Mara imekuwa mwenyeji wa kikao cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Kampuni na Taasisi Binafsi Tanzania (SHIMMUTA) Taifa kilichofanyika kwa mara ya kwanza mkoani Mara leo Februari 10, 2023.

“Tunaishukuru Barrick kama mwanachama na mdau wetu wa SHIMMUTA kukubali ombi letu la kuja kufanya kikao hiki hapa, hakika kikao kimekuwa cha mafanikio,” amesema Mwenyekiti wa SHIMMUTA Taifa, Roselyne Massam.

Kwa mujibu wa Katibu wa SHIMMUTA Taifa, Dkt Maswet Crescent Masinda, kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Taifa, ilani ya chama tawala - CCM na maagizo ya Mlezi wa SHIMMUTA ambaye ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yanayolitaka shirikisho hilo kuhakikisha kuwa linawafikia wadau wake kuhamasisha ushiriki wa watumishi katika michezo.

Viongozi hao wa SHIMMUTA wamesema michezo mahali pa kazi ni muhimu katika kujenga afya na kuongeza ari ya kazi na ufanisi kwa watumishi wa mashirika, kampuni na taasisi za umma na binafsi.

Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Kimefunguliwa na Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi huo, Jan Jacobs na kuongozwa na Mwenyekiti wa SHIMMUTA Taifa, Roselyne, katika kuweka mikakati, kufanya tathmini ya mashindano ya michezo mbalimbali yatakayoendeshwa na shirikisho hilo, lakini pia kuamua yafanyike lini na wapi mwaka huu.
Pia kikao hicho kililenga kujua jinsi Barrick ilivyojipanga kuhudhuria mashindano ya SHIMMUTA mwaka huu, ambapo Meneja Rasilimali Watu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Emmanuel Msaki amethibitisha kuwa wamejipanga kushiriki kikamilifu.

“Hatukuweza kuhudhuria mashindano ya SHIMMUTA kwa miaka mitatu iliyopita kutokana na mlipuko wa corona uliokuwepo, ila niwahakikishie kuwa tutakuwa pamoja kwani kwenye bajeti zetu mwaka huu tumeweka na ya kutuwezesha kushiriki,” Msaki ameiambia Kamati hiyo.

Naye Meneja Usalama na Afya Mahali pa Kazi wa mgodi wa North Mara, Dkt Nicholas Mboya - katika kukazia kauli ya Msaki, amesema “Mwaka huu tunarudi kuwa sehemu ya familia ya SHIMMUTA kwa maana ya kushiriki kwenye michezo.”

Mwenyekiti wa SHIMMUTA Taifa, Roselyne, amesema ushiriki wa watumishi wa Barrick kwenye mashindano hayo utakuwa muhimu na wenye tija kwa shirikisho hilo.

Kesho Februari 11, 2023, wajumbe Kamati hiyo ya SHIMMUTA watapata fursa ya kuongozwa na wenyeji wao kutembelea na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, zikiwemo za utekelezaji wa miradi ya huduma za kijamii katika vijiji vinavyopakana nao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages