NEWS

Monday 20 February 2023

Benki ya Azania yaipiga jeki Shule ya Msingi Kenyamonta kwa msaada wa vifaa vya ofisiNa Mwandishi Wetu, Serengeti
----------------------------------------------

BENKI ya Azania imekabidhi msaada wa vifaa vya ofisi kwa Shule ya Msingi Kenyamonta yenye wanafunzi 779 wilayani Serengeti, Mara kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuinua kiwango cha elimu, hasa ya msingi nchini.

Hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo ilifanyika shuleni hapo wiki iliyopita, ambayo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Makuruma.

Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni sita vimejumuisha mashine ya kisasa ya kudurufu (photocopy machine), kompyuta, mashine ya kupiga chapa (printer), machine ya kuchana na kubana karatasi na vifaa vya kupunguza nguvu ya umeme unaozidi (stabilizers).

Vilikabidhiwa kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Serengeti, Cosmas Qamara aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya, Dkt Vincent Mashinji.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, Qamara aliishukuru Benki ya Azania kwa kutoa msaada huo na kuzitaka benki zingine kuiga mfano huo.

“Tunawashukuru sana Benki ya Azania kwa kutushika mkono katika kuunga mkono jitihada za Serikali na hasa katika sekta hii ya elimu, sisi kama Serikali tunathamini msaada huu kwa kuangalia zaidi matokea yatakayopatikana kutokana na urahisi watakaopata walimu katika kuandaa mitihani yenye lengo la kuwanoa zaidi wanafunzi wa hapa Kenyamonta.

“Na pia nitoe wito kwa walimu na watendaji ambao wataenda kutumia vifaa hivi wavitumie kwa uangalifu ili viweze kudumu na kuongeza tija katika utendaji wao wa kazi,” alisema Qamara.

Naye Meneja wa Benki ya Azania Tawi la Lamadi, Muhidin Mjuvi alisema benki hiyo imeguswa na uhitaji wa vifaa hivyo katika shule hiyo - japokuwa Serikali ya Wilaya imejitahidi kutatua kwa kiasi kikubwa.

Mjuvi alisema msaada huo ni muendelezo wa Benki ya Azania katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza sekta ya elimu nchini.

“Sisi kama taasisi ya fedha tumeona tunalo jukumu la kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutatua kero na changamoto mbalimbali za wananchi katika sekta ya elimu, hivyo tulipoona fursa ya kuwashika mkono tukafanya hivyo bila kusita, ikizingatiwa kuwa Benki ya Azania ni moja ya benki ambazo hurudisha sehemu ya faida yake kwa jamii (CSR) kupitia sekta mbalimbali. Tunaamini vifaa hivi vitakwenda kutatua changamoto iliyokuwepo na sasa kiwango cha ufaulu kitaongezeka,” alisema Mjuvi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Makuruma, iliwalazimu walimu kwenda maeneo ya Mugumu au Musoma mjini - umbali wa kilomita zaidi ya 60 ili kuweza kupata huduma ya kuchapa na kudurufu mitihani ya wanafunzi.

Hivyo sasa kupitia msaada huo ni wazi kuwa Shule ya Msingi Kenyamonta itaongeza ufaulu katika wilaya ya Serengeti yenye shule za msingi za Serikali zipatazo 133.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages