NEWS

Monday 20 February 2023

Kishindo cha Mbunge Waitara Nyanungu, wananchi wakubali kutoa ushirikiano vigingi vya mpaka wa Hifadhi ya Serengeti viwekwe kumaliza mgogoro uliopo



Na Mara Online News
---------------------------------

WAKAZI wa Kata ya Nyanungu wilayani Tarime, Mara wameahidi kushiriki kikamilifu katika utambuzi na uwekaji wa vigingi vya mpaka unaotenganisha vijiji vyao na Hifadhi ya Taifa Serengeti ili kumaliza mgogoro uliopo.

Wananchi hao walitoa ahadi hiyo mbele ya Mbunge wao wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (pichani juu kulia), alipohutubia mkutano mkubwa wa hadhara wa wakazi wa vijiji vya Kegonga na Nyandage katani hapo, jana Februari 19, 2023.

Walimhakikishia mbunge huyo kuwa wako tayari kukutana, kuzungumza na kufikia makubaliano ya pamoja na viongozi husika, wakiwemo wenye dhamana ya ardhi, maliasili na utalii watakaokwenda kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kugombea mpaka wa vijiji vyao na hifadhi hiyo.

Huku akiwapongeza wananchi hao kwa kuonesha utayari huo, Mbunge Waitara naye aliwaahidi kushughulikia haraka iwezekanavyo hatua ya kuhakikisha viongozi husika kutoka wizara zenye dhamana wanafika katani Nyanungu ‘kukata mzizi wa fitina’.

Aliongeza kuwa katika hatua hiyo atahakikisha viongozi wa vijiji na kata, wazee maarufu na wananchi wa kawaida wanashirikishwa kikamilifu katika kufikia suluhisho la kudumu la mgogoro uliopo baina ya pande hizo mbili.

Wazee maarufu wakifuatilia hotuba ya Mbunge Waitara mkutanoni

Hatua ya kumaliza mgogoro uliopo itasaidia kuboresha uhusiano na ujirani mwema kati ya wanavijiji hao na Hifadhi ya Taifa Serengeti, kwa maendeleo yao ya kijamii, kiuchumi na uhifadhi endelevu wa wanyamapori na mazingira hai.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages