NEWS

Monday, 6 February 2023

Mbunge Waitara: Barrick North Mara ni wadau wakubwa wa maendeleo ya wananchi Tarime Vijijini, nitaendelea kushirikiana nao



Na Mwandishi Wetu, Tarime
--------------------------------------------

MBUNGE wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (CCM), amesema hawezi kujitenga, au kubeza Mgodi wa Dhababu wa Barrick North Mara ambao unatoa mchango mkubwa wa maendeleo ya wananchi katika jimbo hilo.

Waitara ametolea mfano mabilioni ya fedha ambazo kampuni ya Barrick imetoa hivi karibuni kugharimia miradi ya kijamii, kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika jimbo hilo lenye vijiji 88.

“Eti wananiambia nisiende kwenye mgodi, mimi ni mbunge, mimi siyo mshamba. Serikalii ina asilimia 16 kwenye mgodi, halafu wametupa shilingi bilioni 5.6 ziko mtaani [akimanisha zinatekeleza miradi ya maendeleo].

“Mwezi wa pili [Februri 2023] wanatoa tena shilingi bilioni nane na mwezi kwanza mwakani [2024] wanatoa tena bilioni sita,” Mbunge huyo alisema katika sehemu ya hotuba yake wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika kimkoa kwenye uwanja wa “Shamba la Bibi” mjini Tarime, wiki iliyopita.
Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara.

Taarifa zilizopo zinaonesha kampuni ya Barrick ilianza kutenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya kugharimia mradi ya kijamii katika vijiji 11 vinavyozunguka mgodi wa North Mara mwaka 2019, ambapo kwa mara ya kwanza ilitenga Dola milioni 2.5.

Aidha, kampuni hiyo ilitenga Dola milioni 1.8 kwa ajili ya kugharimia miradi ya CSR kwa mwaka 2020, Dola milioni 1.8 pia kwa mwaka 2021 na Dola milioni 1.18 kwa mwaka uliopita wa 2022.

Mwaka jana kwa mara ya kwanza, vijiji 77 vya jimbo la Tarime Vijijini ambavyo havipo jirani na mgodi huo vilipata asilimia 30 ya ‘keki’ ya mabilioni ya CSR, jambo ambalo Waitara analitaja kuwa ni la kihistoria katika uongozi wake.

Aliwakosoa vikali baadhi ya wanasiasa aliowaita washamba wanaosema kuwa hapaswi kuhudhuria shughuli za kimaendeleo zinazofanywa na mgodi wa North Mara unaoendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia kampuni ya Twiga Minerals.

Waitara alisema mbali na kutoa mabilioni ya CSR, uwepo wa mgodi huo unatoa fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wakiwemo vijana na wanawake, huku pia ukisaidia kujenga miradi mingine mbalimbali ya kimaendeleo.

“Wanajenga uwanja wa mpira, halafu wanajenga kilomita 45 za barabara, halafu wanapeleka miradi ya kilimo kwa vijana kwenye kata, halafu na akina mama wanauza mchele huko. Unaleta ushamba wako mimi niu- copy (niuige),” alisema mbunge huyo ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa wabunge wachakapa kazi mkoani Mara, hasa katika kufuatilia miradi ya maendeleo ya wananchi.

Kuhusu fidia za mali mbalimbli za wananchi wanohamishwa kupisha upanuzi wa shughuli za mgodi wa North Mara, Waitara alisema wengi wameshalipwa shilingi zaidi ya bilioni 20 na wengine wanaendeleo kujitokeza kulipwa baada ya kuelimishwa na kamati maalumu iliyoundwa na serikali kuhakikisha kila upande unapata haki inayoustahili.

Mbunge Waitara ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri kwenye wizara mbalimbali katika miaka ya hivi karibuni, alisema ataendelea kufanya kile alichokita siasa safi - akilenga kuacha alama isiyofutika ya maendeleo ya miradi ya kihistoria Tarime Vijijini.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages