NEWS

Monday 6 February 2023

MUWASA ilivyojipanga kuboreshea wananchi huduma ya maji katika miji ya Mugumu, Tarime


Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, Mhandisi Nicas Mugisha.

Na Waandishi Wetu, Musoma
------------------------------------------

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) imejiwekea mipango mikakati ya muda mfupi ya kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa miji ya Mugumu na Tarime mkoani Mara.

MUWASA imechukua hatua hiyo baada ya kukabidhiwa majukumu ya mamlaka za maji Mugumu, Tarime na Shirati, ikiwa ni utekelezaji wa Tangazo la Serikali (Government Notice - GN) Na. 353 lililochapishwa kwenye gazeti la Serikali Mei 20, 2022.

Hivyo mamlaka za maji Mugumu, Tarime na Shirati sasa zimegeuzwa kuwa matawi ya MUWASA.

Uvunjaji wa mamlaka za maji za miji hiyo na nyingine nchini, ni mkakati wa Wizara ya Maji na Serikali - wa kuboresha huduma ya maji, baada ya kuona zimekuwa haziwezi kujiendesha na kukidhi mahitaji ya wananchi.

“Serikali imechukua hatua hii kwa sababu mamlaka kubwa za maji (ikiwemo MUWASA) zina uwezo wa rasilimali fedha na watu [watumishi] kwa ajili ya kuboreshea wananchi huduma ya maji,” amesema Mkurugenzi Mtendaji (MD) wa MUWASA, Mhandisi Nicas Mugisha katika mahojiano maalumu na Sauti ya Mara ofisini kwake mjini Musoma juzi.

Anaongeza “Kwetu sisi tunaona tumebebeshwa mzigo mkubwa unaotupa changamoto ya kuwaboreshea wananchi huduma ya maji lakini kazi lazima iendelee.”

Mhandisi Mugisha anasema tayari MUWASA imechukua hatua mbalimbali zinazolenga kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa miji ya Mugumu na Tarime ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za huduma hiyo tangu nchi ipate uhuru.

Mfano pamoja na mambo mengine, MUWASA imefanikiwa kukomesha tatizo la kukatiwa umeme ambalo limekuwa likiikabili Mamlaka ya Maji Mugumu kutokana na kushindwa kulipa bili ya nishati hiyo, hali ambayo imekuwa ikikwaza usambazaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

“Kwa sasa suala la kukatiwa umeme Mugumu halipo. Sisi [MUWASA] tunalipa bili ya umeme na kununua dawa ya kutibu maji kwa wakati, tumepunguza mgawo wa maji na huduma zimeboreka,” anasema Mhandisi Mugisha.

Licha ya MUWASA kurithi deni la shilingi milioni 200 kutoka iliyokuwa Mamlaka ya Maji Mugumu, hilo haliwakatishi tamaa ya kufanya kila linalowezekana ili kufikia malengo ya Wizara ya Maji ya kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.

“Mapungufu yote lazima tuyamalize. Mkatati mwingine tulio nao ni kupanua mtandao wa maji ya bomba ili kuongeza idadi ya watumia maji na mapato. Hii itatuwezesha kupata fedha za kuendesha mamlaka,” anasema MD huyo wa MUWASA.

Idadi ya watu wanaopata huduma ya majisafi na salama ya bomba chini MUWASA katika mji wa Mugumu ni 41,443 sawa asilimia 64.5 ya wakazi wa mji huo, kwa mujibu wa Mhandisi Mugisha.

Anasema tayari mamlaka hiyo imeomba shilingi milioni 300 kutoka wizarani za kununua bomba kwa ajili ya kupanua mtandao wa maji katika mji wa Mugumu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa muda mfupi wa kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa mji huo.

MUWASA pia itaboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi wake waliopo Mugumu, ambapo pamoja na mambo mengine, watapewa vitendea kazi vikiwemo pikipiki na gari.

“Pia tuna mpango wa kujenga ofisi ya kisasa ya MUWASA Tawi la Mugumu,” anadokeza MD Mugisha.

Mikakati kuboresha
maji mji wa Tarime
Kwa upande wa mji wa Tarime, MUWASA ina mpango wa kujenga chujio la maji (simple water treatment plant) katika bwawa la Nyandurumo ili kuwaondolea wananchi kero ya muda mrefu ya majitope.

“Tunatarajia ujenzi wa chujio hilo uanze haraka iwezekanavyo na tutatumia fedha zetu za ndani [za MUWASA], tunatarajia liwe limekamilika ndani ya miezi mitatu,” anasema Mhandisi Mugisha.

“Kwa sasa asilimia 45 ya wakazi wa mji wa Tarime ndio wanaotumia maji ya bomba kutoka kwenye visima na bwawa la Nyandurumo,” anabainisa.

Wakati huo huo MUWASA imeomba shilingi milioni 370 kwa ajili ya kutekeleza mpango mkakati wake wa muda mfupi wa kupanua mtandao wa maji katika mji wa Tarime, kwa mujibu wa MD Mugisha.

Lakini pia habari njema ni kwamba kuna mradi unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi zaidi ya milioni 500 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya mapambano dhidi ya UVIKO-19, ambao utawezesha zaidi watu 4,000 kuanza kupata huduma ya maji.

Utekelezaji wa mradi huo, kwa mujibu wa Mhandisi Mugisha, unahusisha ujenzi wa tenki la maji, kufunga pampu na umeme kwenye kisima cha maji na kutandaza mabomba kwa urefu wa kilomita 25.

“Mradi huu wa UVIKO unatekelezwa katika kata ya Sabasaba na uko hatua za mwisho za kukamilika,” anasema MD wa MUWASA, Mhandisi Mugisha.

Suluhisho la kudumu
la maji mji wa Tarime
Hata hivyo Mhadishi Mugisha anasema mwarobaini wa tatizo la ukosefu wa majisafi na salama ya kutosha katika mji wa Tarime, ni mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria unaojulikana kwa jina la Rorya na Tarime.

Anasema utekekezaji wa mradi huo tayari umeanza na kazi inaendelea katika eneo la chanzo chake wilayani Rorya.

Mradi huo ambao umetengewa shilingi bilioni 134 kutoka serikalini, unatekelezwa na mkandarasi kutoka China anayejulikana kwa jina la China Civil Engineering and Construction Company (CCECC).

“Tayari mkandarasi amepewa malipo ya awami (advance payment) ya shilingi bilioni 20 na utekelezaji wa mradi umeshaanza,” anasema Mhandishi Mugisha na kuongeza kuwa mradi huo utatekelezwa kwa miezi 30 na unatarajiwa kukamilika Machi 2025 na kuwezesha wananchi kupata majisafi na salama kutoka Ziwa Victoria.

Akihutubia mkutano wa hadhara baada ya makabidhiano na mkandarasi eneo la ujenzi wa mradi wa maji wa Rorya na Tarime kijijini Nyang’ombe, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aliahidi kutoa ushirikiano na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo.

“Mimi Jumaa Aweso na timu yangu katika Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo katika kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati, ili wananchi wapate huduma ya majisafi na salama… hatutacheka na mkandarasi, tutacheka na maji,” alisema.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

Waziri Aweso alibainisha kuwa mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya chama tawala - CCM na kwamba wakazi wa vijiji 32 katika kata 10 wilayani Rorya na kata nane wilayani Tarime watanufaika na mradi huo.

Waziri huyo alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba vijana wanaopata ajira katika utekelezaji wa mradi huo kuwa waminifu, kwa kuepuka kuuhujumu kwa namna yoyote ile.

“Pasitokee hujuma, tutakuwa hatujitendei haki,” alisema Waziri Aweso na kuwaomba wananchi kumpa ushirikiano mkandarasi husika, ili atekeleze mradi huo kwa urahisi.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages