Na Mwandishi Wetu
-----------------------------
VIJIJI vilivyo jirani na Hifadhi ya Taifa Serengeti katika kata ya Nyanungu wilayani Tarime vina mlima wenye mandhari ya kipekee, unaofaa kwa uwekezaji wa hoteli za kitalii.
Hata hivyo bado hakuna uwekezaji wowote katika mlima huo ambao ukiwa juu yake unatazama vizuri muonekano wa hifadhi hiyo upande wa Kaskazini unaokuwa na makundi makubwa ya wanyamapori, wakiwemo nyumbu misimu ya utalii.
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee sasa anawataka wakazi wa vijiji hivyo ambavyo ni Kegonga na Nyandage kuona umuhimu wa kuruhusu uwekezaji wa hoteli na kambi za kitalii katika eneo hilo.
RC Mzee ametoa pendekezo hilo mara baada ya kutembelea eneo hilo jana, akifuatana na viongozi mbalimbali wakiwemo wa CCM mkoa, wilaya na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa lengo la kusuluhisha mgogoro kati ya wananchi na hifadhi hiyo bora Afrika.
Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi hao wa Nyanungu kutunza mlima huo badala ya kuendelea kuutumia kwa shughuli za kilimo cha kujikimu, akiwapa mfano wa jinsi upande wa nchi jirani umetumia mlima kama huo kwa shuguli za kitalii ili kujikwamua kiuchumi.
“Tuangalie majirani zetu, wao wameruhusu kufanya shughuli za kitalii na kwa hiyo wanapata pesa. Sasa sisi tutafanyaje shughuli za kitalii wakati tunalima pale badala ya kuweka camp sites?” amehoji mkuu huyo wa mkoa.
Ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuweka mpango wa kupata wawekezaji wa hoteli za kitalii katika eneo hilo.
RC Mzee amehimiza pia utunzaji na uhifadhi wa uoto wa asili wa eneo hilo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Pia Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi hao kuheshimu mpaka wao na Hifadhi ya Serengeti ili kuepusha migogoro isiyo na tija, badala yake wajikite kujenga mahusiano na ujirani mwema kwa maendeleo yao ya kiuchumi, kijamii na uhifadhi.
“Maagizo ya serikali, mheshimu mpaka wa hifadhi. Viongozi wengi walikuwa hawajafika katika eneo hili na mimi pia nilikuwa sijafika hapa ila leo nimefika na viongozi wengine.
“Hapa ninyi ni matajiri lakini mnajiletea umasikini wenyewe, hapa ambapo kuna nyumba zingejengwa hoteli za kitalii mngekuwa matajiri. Mnajikosesha utajiri,” amesisitiza mkuu huyo wa mkoa.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patrick Chandi amekazia hoja hiyo ya kutenga milima hiyo kwa ajili ya uwekezaji wa kitalii na kuiomba TANAPA kupeleka wawekezaji wakubwa.
“Hii sehemu ni utajiri mkubwa, nashauri TANAPA ilete wawekezaji wakubwa ndani ya kijiji hiki wajenge hoteli katika milima hii - serikali ya kijiji ikusanye hela, kila mzungu akiingia analipa Dola 30, mtajikuta mnapata fedha nyingi, hili eneo tulifanye la uwekezaji,” amesema Chandi.
Mwenyekiti Chandi (aliyeinua mkono juu) akisisitiza hoja hiyo kwa wananchi hao
Akisisitiza zaidi kuhusu uwekezaji huo, Chandi ametolea mfano kijiji cha Natta kilichopo wilaya jirani ya Serengeti - akisema kina milima miwili midogo kuliko iliyopo Nyanungu, ambayo imejengwa hoteli za kitalii zinazokiingizia shilingi bilioni tatu kila mwaka.
Katika hatua nyingine, RC Mzee amekemea kitendo cha hivi karibuni cha mauaji ya askari wa uhifadhi katika eneo hilo kwa mshale wa sumu, akiwataka wananchi wa maeneo hayo kutorudia kufanya vitendo kama hivyo kwani havikubaliki.
Aidha, RC Mzee amewakosoa vikali watu wanaopendekeza kuwa wananchi hao waruhusiwe kutembelea umbali wa kilomita zaidi ya 20 kupeleka mifugo yao kunywa maji katika mto Mara.
“Vitu vingine wananchi msipelekeshwe na watu ambao wanawadanganya kwa faida zao. Kaa mjitafakari,” amesisitza kiongozi huyo wa mkoa.
Katika ziara hiyo iliyolenga kusuluhisha mgogoro kati ya wananchi wa vijiji vya katani Nyanungu na Hifadhi ya Taifa Serengeti, RC Mzee na Mwenyekiti Chandi walifuatana na viongozi mbalimbali wakiwemo Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, William Mwakilema, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele na Mwenyekiti wa CCM Wilaya hiyo, Marwa Daudi Ngicho, miongoni mwa wengine.
Meja Jenerali Mzee (mwenye suruali ya bluu) akisalimiana na Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, William Mwakilema walipokutana katika ziara hiyo. Wengine ni viongozi mbalimbali kutoka shirika hilo na Mkuu wa Wilya ya Tarime, Knali Mntejele. (Picha zote na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment