NEWS

Sunday, 11 January 2026

BUWSSA yafanya uwekezaji mkubwa kukabili upotevu wa maji Bunda Mjini



Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, akikata utepe wakati wa kuweka jiwe la msingi Mradi wa Uboreshaji wa Mtandao wa Mabomba kutoka Mingungani hadi Kaswaka wilayani Bunda, mkoani Mara, Januari 7, 2026.

Na Mwandishi Wetu
Mara Online News
------------------------

Kwa muda mrefu, mji wa Bunda mkoani Mara umekuwa na tatizo la upotevu mkubwa wa maji kupitia mabomba chakavu, na hivyo kusababisha hasara na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Lakini sasa tatizo hilo linaelekea kukomeshwa baada ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA) kuja na mpango kabambe wa kuhakikisha upotevu wa maji unabaki historia katika mji huo unaokua kwa kasi.

Kupitia uwekezaji wa kimkakati, BUWSSA imeanza utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Mtandao wa Mabomba kutoka eneo la Mingungani hadi Kaswaka, unaolenga kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 31 ya sasa hadi asilimia 20 inayokubalika kimataifa.

Ni mradi unaobeba matumaini mapya kwa wakazi wa mji wa Bunda, na uthibitisho wa dhamira thabiti ya serikali katika kuboresha huduma za msingi kwa wananchi.

Serikali kupitia Wizara ya Maji imeendelea kutoa msukumo wa kisera na kifedha kukabiliana na upotevu wa maji, hasa pale ambapo uongozi, taaluma na uwajibikaji vinapokutana.

Katika kudhihirisha dhamira hiyo, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, Januari 7, 2026 aliweka jiwe la msingi la mradi huo wa Uboreshaji wa Mtandao wa Bomba kutoka Mingungani hadi Kaswaka wenye thamani ya shilingi bilioni 1.4.

Mhandisi Kundo alisema matarajio ya serikali ni kwamba mradi huo wa kimkakati utawezesha kupunguza upotevu wa maji na kunufaisha wakazi 227,446 wa kata zote za mji wa Bunda.

Alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Esther Bulaya, kwa ushirikiano wake wa karibu na serikali katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati, akisisitiza kuwa usimamizi wa karibu wa viongozi wa wananchi una mchango mkubwa katika mafanikio ya miradi ya maendeleo.

Awali, akiwasilisha kero za wananchi kwa Naibu Waziri Kundo, Bulaya alisema mradi huo umejibu kilio chake cha muda mrefu cha kuuondoa mji wa Bunda katika orodha ya maeneo yenye upotevu mkubwa wa maji, hali iliyokuwa ikiathiri ufanisi wa upatikanaji wa huduma hiyo.

Aidha, alisema ana imani kubwa na usimamizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa BUWSSA, Esther Gilyoma, akieleza kuwa tangu aanze majukumu yake ameonesha uwezo na uthubutu wa kupambana na upotevu wa maji, hatua iliyosaidia kupunguza kiwango hicho kutoka asilimia 45 hadi 31 ya sasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Gilyoma alisema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 50, huku akiishukuru serikali kwa kuendelea kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 28 katika miradi mbalimbali ya maji wilayani Bunda.

Gilyoma alisisitiza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutakuwa hatua muhimu katika safari ya BUWSSA ya kuhakikisha maji yanayozalishwa yanawafikia wananchi bila kupotea, na hivyo kuboresha huduma, kuongeza mapato ya Mamlaka na kuinua ustawi wa jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages