NEWS

Monday 13 February 2023

RUWASA yajenga uelewa wa pamoja na viongozi mkoani Mara kuhusu utoaji huduma ya maji vijijiniNa Mwandishi Wetu, Musoma
----------------------------------------------

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara imeandaa kikao cha kujenga uelewa wa pamoja baina yake, Sekretarieti ya Mkoa na viongozi mbalimbali kuhusu mwelekeo mpya wa utoaji wa huduma za maji vijijini, chini ya Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya Mwaka 2019.

Kikao hicho kilifanyika mjini Musoma juzi, ambapo kiliongozwa na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee, ambaye alisema Serikali ya Awamu ya Sita imetoa shilingi zaidi ya bilioni 23 kwa ajili ya kugharimia utekelezaji na usimamizi endelevu wa miradi ya maji katika mkoa wa Mara kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

RC Mzee aliitaka RUWASA kuhakikisha inasimamia vizuri utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Mara, ili kutimiza lengo la Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan la kumtua mama ndoo ya maji kichwani.

Alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuelekeza mabilioni ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Mara, huku akimpongeza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwa juhudi kubwa anazofanya kuhakikisha huduma za maji kwa wananchi zinaboreshwa nchini.

Hata hivyo Mzee alisema bado mkoa wa Mara ambao unapakana na Ziwa Victoria una hitaji la kuboreshewa huduma za maji, ili kukidhi mahitaji ya wananchi na lengo la serikali, lakini pia kutekeleza ilani ya chama tawala - CCM.

“RUWASA mna jukumu kubwa la kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji na kuepusha ubadhirifu dhidi ya miradi hiyo,” alisema kiongozi huyo huyo wa mkoa.

RC Mzee akizungumza kikaoni

Kuhusu wakandarasi wa miradi ya maji, RC Mzee aliitaka RUWASA kuhakikisha inajiridhisha kwanza kama wana uwezo wa kutekeleza na kukamilisha miradi kwa wakati, kabla ya kuwapa zabuni.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Lengael Akyoo, mbali na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa jitihada kubwa inazofanya kuboreshea wananchi huduma za maji, alitaka kila mmoja kushiriki katika uhifadhi na ulinzi wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.

“Kwa hiyo watu wote wanaoharibu vyanzo vya maji kwa namna yoyote ile lazima wachukuliwe hatua kali kwa mujibu wa sheria,” alisema Akyoo.

Awali, akitoa taarifa fupi katika kikao hicho, Kaimu Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mara, Mhandisi Marko Chogero alisema kwa sasa huduma ya maji kwa wananchi wa vijijini inapatikana kwa asilimia 71 katika maeneo wanayohudumia.

“Hadi Januari 2023, asilimia 71 ya wananchi wanaoishi vijijini katika mkoa wetu wa Mara wanapata huduma ya majisafi. Hatua hii imefikiwa kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Mhandisi Chogero.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa miradi ya maji unaendelea katika hatua mbalimbali chini ya usimamizi wa RUWASA mkoani Mara.

Aidha, Mhandisi Chogero alisema hivi karibuni RUWASA Mkoa wa Mara ilisaini mkataba kwa ajili ya ujenzi wa miradi kadhaa ya maji katika wilaya za Bunda na Butiama.

Kwa upande mwingine, alisema RUWASA inamalizia kufanya tathmini ya kuwapata wakandarasi kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa miradi ya maji katika maeneo mengine ya wilaya za Bunda, Tarime na Serengeti.

RUWASA ilianzishwa nchini Tanzania chini ya Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya Mwaka 2019, ili kuongeza, kuboresha na kuwezesha huduma za maji na usafi wa mazingira kwa wananchi vijijini kuwa endelevu.

Majukumu ya RUWASA ni pamoja na kusanifu, kujenga na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maji na uendeshaji wake kupitia vyombo vya kijamii.

Mengine ni kuvijengewa uwezo vyombo vya kijamii vinavyohusika na huduma ya maji (CBWSOs) kwa mafunzo na utaalamu wa uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji.

Pia, kuhamasisha wananchi kuhusu usafi wa mazingira, uhifadhi, utunzaji vyanzo vya maji na kushirikiana na wadau mbalimbali katika huduma za maji na usafi wa mazingira vijijini.

RUWASA mkoani Mara inawashukuru viongozi wa serikali na kijamii, lakini pia waandishi wa habari, kwa ushirikiano mzuri wanaoipatia katika juhudi za kuboresha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi vijijini.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages