NEWS

Monday 13 February 2023

Serikali ya Kijiji cha Nyangoto kujenga soko la kisasa la kwanza Nyamongo



Na Mwandisi Wetu, Nyamongo
-------------------------------------------------

NI “hot cake”. Ndivyo unavyoweza kueleza fursa za ujenzi wa soko jipya la kisasa katika kijiji cha Nyangoto, kilichopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara.

Tayari ujenzi huo umeanza kwa kasi, huku wananchi wakimiminika kuomba eneo la kujenga vibanda vya biashara katika eneo hilo, jirani na ofisi za Serikali ya Kijiji hicho.

“Maombi ya wananchi yalikuwa zaidi ya 480 lakini waliopata maeneo ya kujenga vibanda ni 228 kuzunguka soko hilo, na wengi wao wmeanza kujenga,” Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto, Mwalimu Mwita Msegi aliiambia Sauti ya Mara ilipotembelea eneo hilo, wiki iliyopita.

Gazeti hili lilishuhudia shughuli mbalimbali za ujenzi zikiendelea kwa kasi baada ya Serikalii ya Kijiji kutoa ramani na mfano wa vipanda vya kisasa vinavyotakiwa.

“Tumejenga vipanda vinne vya mfano; viwili vinatazama nje na viwili vingine ndani ya soko. Hili litakuwa ni soko la kisasa na la kwanza Nyamongo,” anasema Mwalimu Msegi.
Mwenyekiti Msegi akionesha shughuli za ujenzi zinazoendelea

Aidha, Serikali ya Kijiji imewekeza shilingi milioni 118 katika ujenzi wa meza za kisasa zipatazo 146 ndani ya soko hilo. Fedha hizo zimetokana na mapato ya ndani ya kijiji hicho, kwa mujibu wa Mwalimu Msegi.

Meza hizo, anasema zitakodishwa kwa wafanyabiashara ya matunda na nafaka, miongoni mwa bidhaa nyingine.

Kwa sasa baadhi ya wafanyabiashara wadogo katika mji mdogo wa Nyamongo, hususan wanawake wanatumia maeneo yasiyo rasmi kuendesha biashara zao - jambo ambalo sasa linaenda kubaki historia.

“Lengo kubwa ni kuwaleta wamama pamoja wafanye biashara zao katika mazingira ambayo ni rafika badala ya mitaani,” anasema Mwalimu Msegi.

Anasema wazo la kujenga soko hilo limebuniwa na Serikali ya Kijiji cha Nnyangoto, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuwezesha wanawake na vijana kiuchumi.

Wakazi wa kijiji cha Nyangoto na mji mdogo wa Nyamongo kwa ujumla wamepokea mradi huo kwa mikono miwili, wakionesha utayari wa kuchangamkia fursa hiyo.
Ujenzi wa vibanda vya soko ukiendelea

“Tumefurahi sana na matarajio yetu ni kufanya biashara ili kuinua kipato chetu. Tunaishukuru sana serikali ya kijiji kwa kuwekeza soko la kisasa hapa,” anasema Ayub Bugingo, mkazi wa kitongoji cha Mnadani kijijini Nyangoto.

Bugingo anaongeza “Wafanyabiashara za kawaida tumekuwa tukihangaika sana kwa kukosa sehemu maalumu ya kuendeshea shughuli zetu za kujipatia kipato, lakini sasa tunafurahi kuona soko linajengwa, wananchi wamegawiwa maeneo ya kujenga vibanda vya biashara, na mimi ni mmoja wao - nimepata eneo la kujenga kibanda namba 45.”

Mkazi mwingine wa Nyamongo aliyebahatika kugawiwa eneo la kujenga kibanda katika soko hilo ni Upendo Faljala. Yeye anaupongeza uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto kwa kuweka utaratibu mzuri wa kugawa maeneo ya kujenga vibanda. “Utaratibu uliowekwa ni mzuri sana, hakuna malalamiko yaliyojitokeza,” anasema.

Ujenzi wa soko hilo unatarajiwa kuongeza mwingiliano wa watu, mzunguko wa fedha, kuinua uchumi na hivyo kuchangia uboreshaji wa hali ya maisha ya wakazi wa kijiji cha Nyngoto na mji wa Nyamongo kwa ujumla.

Soko hilo, kwa mujibu Mwalimu Msegi, unatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika kufikia Aprili mwaka huu.

Mwenyekiti huyo wa Serikali ya Kijiji cha Nyangoto anahitimisha mazungumzo yake na Sauti ya Mara kwa kuwakaribisha wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya Nyamongo kujitokeza kutumia soko hilo katika kukuza biashara zao na kuinua uchumi wao.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages